Na Mwandishi wetu, Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi, amezindua rasmi zoezi la usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo 6 katika mkoa huo, huku akiwataka Wananchi kuchangamkia fursa ya matumizi ya nishati safi kama njia mbadala ya kupunguza uharibifu wa mazingira.
Kenani amesema kuwa Uharibifu wa Mazingira umechangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya kuni na mkaa na kwamba lengo la Serikali ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kulinda afya za Watanzania pamoja na kutunza mazingira.
Amewataka Wananchi wa mkoa wa huo kununua mitungi hiyo ya gesi pamoja na vifaa vyake ambavyo vinasambazwa na kampuni ya ORYX Gas.
“Utekelezaji wa Mradi huu, unaunga mkono Mpango Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo, lengo ni kuhakikisha kuwa angalau asilimia 80 ya Watanzania, wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.” amesema Kihongosi.
Naye Mhandisi wa Miradi ya Nishati Safi kutoka REA, Geofrey Gedo, amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha Wanachi waliopo katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetenga fedha, takribani shilingi za Kitanzania milioni 325 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya kuhamasisha matumizi ya gesi ya kupikia (LPG) kwa mkoa wa Simiyu." Amesema na kuongeza.
“Mradi pia, unalenga katika kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti, ambapo takribani hekta laki 4 (400,000) hukatwa kila mwaka; wakati asilimia 63.5 ya kaya hutumia kuni kama chanzo kikuu cha nishati na asilimia 26.2 hutumia mkaa."
Mhandisi, Gedo ameongeza kuwa mitungi 16,275 itauzwa kwa bei ya punguzo ya asilimia 50 ambayo ni shilingi 20,000 katika mkoa wa Simiyu na kila wilaya ipata mitungi 3,255.
Ameongeza kuwa ili Wananchi wa Simiyu wapate mitungi hiyo wanatakiwa kuwa na kitambulisho cha NIDA pamoja na shilingi (20,000) na watakapofika katika vituo vya kuuzia mitungi hiyo wataulizwa majina yao, jinsia; namba ya nida; mkoa, wilaya, kata, kijiji na kitongoji /mtaa anapoishi.
“Natoa wito kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi ili wanunue kwa bei ya punguzo na hata baada ya gesi kuisha; waendelee kutumia nishati safi, ikiwemo gesi.
Wilaya za mkoa Simiyu zitakazonufaika na usambazaji huo ni pamoja na wilaya ya Maswa, Bariadi, Itilima, Meatu na Busega.
Aidha, Usambazaji wa mitungi hiyo ya gesi unatekelezwa kwa pamoja kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited, ambapo Wananchi wanapata fursa ya kukunua mitungi hiyo gesi ya kilo 6 kwa shilingi (20,000); bei ya ruzuku na kiasi kilichobaki kitalipwa na Serikali kupitia REA.
Mwisho.
Wananchi wakiwa kwenye foleni Kwa ajili ya kupata mitungo ya Gesi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi.
إرسال تعليق