Na Derick Milton, Bariadi.
Katika kuhakikisha inaunga mkono juhudi za serikali na
wananchi za kuboresha mazingira kwenye sekta ya Elimu nchini Benki ya NMB
imetoa mabati 400 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa katika shule za
Msingi Mwamijondo na Banemhi.
Shule hizo zilizoko katika Halmashauri ya Wilaya ya
Bariadi Mkoani Simiyu zimepatiwa mabati hayo yenye thamani ya Sh Milioni 14.4,
ambapo katika shule ya Mwamijondo NMB imetoa bati 260 na Banemhi bati 140.
Akikabidhi vifaa hivyo katika hafla iliyofanyika jana
kwenye shule ya Msingi Mwamijondo, Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Restus
Assenga alisema kuwa mabati hayo yatakamilisha ujenzi wa vyumba 8 kwenye shule
zote mbili.
Alisema kuwa mbali na serikali kuendelea kuboresha mazingira
ya ufundishaji na ujifunzaji kwenye sekta ya elimu, NMB kama mdau umekuwa
wajibu wake kuhakikisha inaunga mkono juhudi hizo za serikali.
“ Pamoja na mambo makubwa yote ambayo serikali yetu
inaendelea kufanya, sisi kama wadau tunawajibu wa kuunga mkono juhudi hizo za
maendeleo kwa kusaidia jamii, kwani wateja wetu pia wapo kwenye hizo jamii,”
alisema Assenga.
Alisema kuwa NMB inatambua kuwa elimu ndiyo nguzo kuu
ya maendeleo kwa taifa, jambo ambalo limekuwa chachu kwa taasisi hiyo katika
kuhakikisha inaunga mkono juhudi za serikali kuboresha sekta hiyo.
Akipokea vifaa hivyo Mbunge wa Jimbo hilo na Naibu
Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Andrea aliwashukuru NMB kwa vifaa hivyo ambavyo
alieleza vitakwenda kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo.
Mhandisi Kundo alisema kuwa uwepo wa mazingira mazuri
ambayo yamefanywa na serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamewezesha taasisi
za kifedha nchini kufanya kazi zao na kupata faida ambayo imekuwa neema kwa
wananchi.
“ Bila ya mazingira mazuri ya kufanya kazi zao NMB
wasingelileta vifaa hivyo, mazingira yamekuwa mazuri ndiyo maana leo tunapokea
hivi vifaa ambavyo vitaboresha mazingira ya shule zetu,” alisema Mhandisi
Kundo.
MWISHO
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment