Na Samwel Mwanga,Simiyu.
ULINZI wa maadili hasa kwa vijana wa kiume dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia,ikiwa ni pamoja na kufanyiwa vitendo vya kulawitiwa ni suala nyeti linalohitaji hatua madhubuti kutoka kwa jamii,serikali na taasisi mbalimbali.
Hayo yameelezwa leo alhamisi,April 4,2025 na Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi wakati akizungumza na Simiyupress club blog kwa njia simu juu ya kulinda maadili hasa kwa vijana wa kiume kutoingiliwa kinyume na maumbile.
Amesema kuwa uhalisia wa tatizo hilo katika jamii watoto wa kiume ni waathirika wa ukatili wa kijinsia lakini mara nyingi tatizo hili halizungumzwi kwa kina.
Amesema kuwa mara nyingi wanaofanya vitendo hivyo ni watu wa karibu kama wanafamilia,walimu na majirani na watoto hao wamekuwa waoga wa aibu hivyo huwafanya waathirika wengi washindwe kutoa taarifa.
“Nazidi kusisitiza tulinde maadili hasa kwa vijana wa kiume kutoingiliwa kinyume na maumbile,tuwalinde watoto wa kiume,”amesema.
Amesema kuwa licha ya vitendo hivyo kutoripotiwa kuwepo katika mkoa huo lakini ni vizuri kwa jamii kuelezwa ili iweze kuchukua hatua kwa kuimarisha malezi mema kwa vijana wao hasa wa kiume.
“Katika nchi yetu haya mambo yanakatazwa na kifungu cha 154 cha kanuni ya adhabu kinakataza vitendo vya sodomia na adhabu yake ni kifungo cha maisha au miaka isiyopungua 30 gerezani,”amesema.
Naye Basila Bruno ni afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Maswa anasema kuwa ni jukumu la jamii na wazazi kuwaelimisha watoto wa kiume kuhusu miili yao na mipaka ya faragha.
“Kuwepo na mazungumzo ya wazi ili watoto wawe huru kutoa taarifa wanaponyanyaswa na jamii ishiriki kuwalinda kwa kufichua wanaotenda vitendo vya ukatili wa kijinsia,”amesema.
Caroline Shayo ni Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa anasema kuwa ni vizuri kutolewa elimu kwa vijana kwa kujenga ufahamu kwa watoto wa kiume kuhusu haki zao na namna ya kujilinda.
“Ni lazima kuchukua hatua ya kuzuia suala hili na njia mojawapo ni pamoja na kuwahamasisha waathirika kutoa taarifa haraka kwa vyombo vya sheria au mashirika yanayosaidia waathirika ili wahusika waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria,”amesema.
Ulinzi wa watoto wa kiume ni jukumu la kila mtu ni muhimu kuendelea kuhamasisha jamii kupinga ukatili wa aina yoyote na kulinda maadili.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment