![]() |
Wananchi wa Mtaa wa Mahina Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wakishuhudia Kondoo waliouawa na Fisi. |
Na Derick Milton, Bariadi.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida Kundi Fisi limevamia
nyumbani kwa Mageni Maduhu mtaa wa Mahina kata ya Somanda Halmashauri ya Mji wa
Bariadi Mkoani Simiyu na kushambulia Kondoo wake 21 na kuwaua.
Tukio hilo limetokea jana April Mosi, 2025 majira ya
saa nne usiku, ambapo fisi hao walivamia kwenye zizi la kondoo hao na
kuwashambulia wote.
Mageni Maduhu akisimulia tukio hilo amesema kuwa lianza
kusikia mlio wa fisi mmoja majira hayo ya usiku, akatoka nje na kuanza
kumkimbiza.
Anasema baada ya kumkimbiza fisi huyo njiani alikutana
na kundi jingine la Fisi ndipo alipoamua kurudi nyumbani na alipoelekea kwenye
zizi la kondoo alikuta damu nyingi na kondoo wake wote wakiwa wamekufa.
“ Kwenye zizi kulikuwemo na Kondoo 30, ambao wameshambuliwa
hadi kufa ni 21 na kondoo wengine 9 hatuwaoni walipo mpaka sasa, Kondoo wengine
walikuwa na mimba na wameuawa, fisi walikuwa wengi sana,” alisema Maduhu.
Mwenyekiti wa Mtaa huo Mangu Mangolyo akizungumzia
tukio hilo amesema kuwa limekuwa tukio la kushangaza kwani halijawahi kusikika
au kuona fisi wanashambulia au kula kondoo wengi kiasi hicho.
Magonlyo amesema kuwa alifika kwenye tukio hilo na
kukuta kweli Kondoo wote wameshambuliwa na kuuawa, ambapo alieleza tukio hilo
linashangaza kwani fisi huwa hawana utaratibu wa kushambulia kondoo wengi kiasi
hicho.
Mkuu wa Wilaya hiyo Simon Simalenga ambaye alifika kwa
ajili ya kushuhudia tukio hilo alisema kuwa mpaka sasa bado wanaendelea na
uchunguzi wa kubaini kama ni kweli fisi ndiyo wametenda tukio hilo au hapana.
Simalenga alitoa pole kwa familia ambayo imekubwa na
tukio hilo, ambapo alieleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza
uchunguzi wa tukio hilo ikiwemo mamlaka ya wanyamapori Tanzania.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ametangaza kuanza rasmi kwa
msako wa Fisi katika maeneo yote yenye vichaka kwenye Halmashauri ya Mji wa
Bariadi, ambapo alieleza wameanza kupata taarifa za uwepo wa wanyama hao.
“ Kwa tukio hili lazima tufanye msako mkali wa kupambana
na wanyama hawa, tutafanya msako kwenye maeneo yote, maana tumeanza kusikia na
kuona uwepo wa hao wanyama kwenye halamshauri ya mji wa Bariadi,” alisema
Simalenga.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amewatahadharisha
wananchi wote ambao wanadaiwa kufuga wanyama hao kuacha mara moja kwani msako
huo utafanyika pia kwa watu wote ambao wanadaiwa kumiliki fisi.
“ Katika opereisheni hii niwatahadharishe wale wote
ambao wanamiliki fisi kwa kuwafuga wajisalimishe mara moja, tutachukua hatua
kali kwa wanaofanya hivyo, “ alisema Simalenga.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment