
Na Samwel Mwanga, Maswa.
KAZI ya ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji lenye uwezo wa kubeba lita milioni mbili linalojengwa katika kijiji cha Hinduki wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imefikia hatua ya asilimia 90, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Tenki hilo linajengwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) likiwa na lengo la kuhudumia wakazi wa mji wa Maswa ili waweze kupata huduma ya maji kwa masaa 24.
Akizungumza April 9,2025 mjini Maswa,Kaimu Meneja Ufundi wa MAUWASA, Martin Masanja na waandishi wa habari waliotembelea ujenzi wa tenki hilo amesema kuwa kazi iliyobaki ni kulifunika tenki hilo na ufungaji wa mifumo ya mabomba ya kuingiza na kusambaza maji kwenye tenki.
Amesema kuwa ujenzi wa tenki hilo ni moja ya utekelezaji wa mipango ya mamlaka hiyo iliyojiwekea kwa musimu wa bajeti ya mwaka 2024/2025 ili kuhakikisha ya kuwa inawapatia wananchi huduma bora ya maji ya toshelevu.
“Mradi huu ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mji wa Maswa na tunaendelea kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati bila kuathiri ubora,”
“Tuliamua kuanza ujenzi wa matenki ya maji mawili,tenki la kwanza tulilijenga katika kilima cha Nyalikungu mjini Maswa lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni moja na limeshaanza kazi na sasa tunakamilisha hili tenki katika kijiji cha Hinduki na tukilikamilisha tutaongeza muda wa upatikanaji wa maji kutoka masaa 12 ya sasa hadi 24,”amesema.
Amesema kuwa kukamilika kwa tenki hilo pia kutasaidia kupunguza gharama za uendeshaji katika mamlaka hiyo kwani walikuwa wakisukuma maji moja kwa moja kutoka katika chanzo cha maji bwawa la New Sola lililoko katika kijiji cha Zanzui wilayani humo kwenda kwa watumiaji.
“Kwa sasa tutakuwa tunasukuma maji na kuyazaja kwenye haya matenki kwa muda wa masaa mawili, halafu tunazima mashine na baadaye tunayaruhusu kwenda kwa wananchi kwa ajili ya matumizi lakini siku za nyuma tulikuwa tunasukuma maji moja kwa moja kwa wananchi kwa kuwasha mashine zinazoendeshwa kwa umeme kwa masaa manane,”amesema.
Amesema kuwa ujenzi huo ulioanza Oktoba 25,2022 unatarajia kukamilika kwa asilimia 100 ifikapo mwezi juni 30 mwaka huu mara baada ya ukaguzi wa mwisho wa kitaalamu kufanyika.
Masanja ameendelea kueleza kuwa gharama za ujenzi wa tenki hilo ni Sh milioni 832.6 na gharama za ulazaji wa bomba ni Sh bilioni 1.3 na ujenzi huo unatekelezwa kwa kutumia mfumo wa Force Account ambapo mafundi wazawa wametumika katika ujenzi huo.
“Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Maji kwa kuweza kutupatia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa tenki hili na mtandao wa bomba ili kuhakikisha wanamtua ndoo mama kichwani,”amesema.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, changamoto za muda kama mabadiliko ya hali ya hewa na ucheleweshaji wa vifaa zimeelezwa kuchelewesha kwa kipindi kifupi utekelezaji wa baadhi ya kazi, ingawa hatua zimechukuliwa kurekebisha hali hiyo.
MAUWASA inawahudumia wananchi wapatao 102,682 katika mji wa Maswa na vijiji vipatao 19.
MWISHO.

إرسال تعليق