MrJazsohanisharma

Wafanyabiashara Bariadi walia kuwekwa Mahabusu Ofisi za Wakala wa Vipimo Simiyu..



Na Mwandishi wetu.


WAFANYABIASHARA wilayani Bariadi Mkoani Simiyu wameiomba Serikali kuingilia kati sakata la Wakala wa Vipimo Mkoani humo kuwakamata na kuwaweka Mahabusu kwenye ofisi za Wakala huo, zilizoko Nyaumata pindi wanapofanya kaguzi mbalimbali za vipimo.


Wafanyabiashara hao wamedai kuwa wamekuwa wakikamatwa kutokana na baadhi ya bidhaa zao ikiwemo nondo, vyuma na saruji kutokuwa ma vipimo sahihi na kutuhumiwa kuwa wanahujumu Taifa.



Wakizungumza kwenye Mkutano uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Sweet dreams hotel, wafanyabishara hao wamesema kuwa wanasikitishwa na kitendo cha Afisa Vipimo wa Mkoa kuwakamata na kuwaweka Mahabusu badala ya kuwapa Elimu sahihi juu ya Vipimo.


"Kule viwandani wanaruhusu nondo zenye urefu wa futi 38, unamkamata mfanyabiashara kapunguza futi mbili ili azifanyie nini?..inchi moja ya vyuma (pipe) inapungua theluthi tunaambiwa tunaihujumu inchi wakati bidhaa imetoka kiwandani, mfanyabiashara naaweza kubeba panga ili aparue ukupunguza nondo au chuma ili apate nini?" Amesema  Hamka Hamka.


Wameeleza kuwa Mamlaka yanavyofanya na Wakala huo ni Makubwa mno badala ya kutoa Elimu na kwamba kuwakamata wafanyabiashara na kuwaweka Mahabusu ya ofisi zao ni kuigombanisha serikali na wafanyabiashara hao.


"Unajiita una Mamlaka ya kuweka wafanyabiashara Mahabusu, polisi imeenda wapi, Mahakama imeenda wapi, ile ofisi ya Wakala wa Vipimo ina Mahabusu?..." Amehoji mfanyabiashara Hamka.


Maria John, amesema Afisa Vipimo wa Mkoa huo alifanya ukaguzi kwenye duka la vifaa vya ujenzi na kuwatoza faini ya shilingi Mil. 20 huku wakiwatishia kuwapeleka mahakamani.


"Walishindwa kuelewana na baba (John Sabu), wakitishia kutupeleka mahakamani...hakutaka maongezi yoyote na mifuko miwili ya saruji alikuwa ameichukua, alisema faini ni shilingi Mil. 20 kama mko tayari tutaongea lakini faini lazima ilipwe" Amesema.


Mwakilishi wa kituo Cha Mafuta Nengelo kilichopo Nkololo, Kuchonke Togoro amesema kuwa kituo chao kilipigwa faini ya shilingi mil. 1.5 licha kufanya mazungumzo na Meneja wa Vipimo Mkoa wa Simiyu.


"Niliitwa ofisini kwake, baada ya kushindwa kuelewana aliniambia twende kituo cha polisi, mimi nikagoma na kumwambia nenda ili polisi waniite, akanifungia ofisini kwake kuanzia saa 3 asubuhi mpaka aliporudi saa 6 mchana" amesema Togoro.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini, Alban Kihula, aliyekuwepo kwenye Kikao hicho amesema kuwa masuala ya mahabusu yako Jeshi la polisi na kama kuna mfanyabiashara ana tatizo, Wakala huo huwasiliana na jeshi la polisi kwa hatua zaidi.


Kuhusu madai ya wafanyabiashara kutozwa faini kubwa, Kihula amewataka wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Simiyu kutumia busara kwa asilimia sabini ili kuondoa migogoro na malalamiko ya wafanyabiashara.


Ameongeza kuwa faini hizo zinatokana na bidhaa zinazokuja kukaguliwa na wakala wa vipimo kutokuwa na vipimo sahihi ikiwemo Uzito, Urefu na Unene.


Mwisho.


Hamka Hamka, Mfanyabiashara kutoka Bariadi.


Mfanyabiashara Maria John akiongea kwenye Kikao cha wafanyabiashara.



Wafanyabiashara wakiwa kwenye Kikao katika ukumbi wa Sweet dreams Hotel mjini Bariadi.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini, Alban Kihula (katikati), akimsikiliza hoja za Wafanyabiashara mjini Bariadi.






Mwakilishi wa kituo Cha Mafuta Nengelo kilichopo Nkololo, Kuchonke Togoro akiongea kwenye Kikao cha wafanyabiashara kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Sweet dreams hotel.
















Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post