Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WANANCHI zaidi ya 10,000 kutoka vijiji vitatu vya Sakwe, Mwangimu na Mwanzoya, wilayani Bariadi Mkoani Simiyu wanatarajia kunufaika na Mradi wa Maji Sakwe unaotekelezwa na Wakala wa Maji ma Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa gharama ya shilingi Bil. 1.04.
Mradi wa Maji Sakwe unatarajia kutoa huduma ya Maji safi na salama kwa wananchi ambao mahitaji yao kwa siku ni lita 269,025, huku chanzo chake kina uwezo wa kukidhi mahitaji ya wananchi 10,761 kutoka katika vijiji hivyo.
Akitoa taarifa ya Ujenzi wa Mradi huo, mbele ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Bariadi, Mhandisi Herry Magoti amesema kuwa katika Mradi huo
wanajenga Tanki lenye ujazo wa lita 135,000 juu ya mnara wa mita 12.
"Mradi unakidhi mahitaji ya wananchi 10,761 sawa na asilimia 100 ya wananchi kutoka vijiji vya Sakwe, Mwangimu na Mwanzoya...Mradi huu utasaidia wananchi kupata Maji safi na salama tofauti na zamani" amesema Mhandisi Magoti na kuongeza.
"Wataondokana na adha ya kutembea umbai mrefu kutafuta Maji pia watapunguza magonjwa yatokanayo na kutumia Maji yasiyo safi na salama, tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa kutoa fedha za Mradi huu".
Diwani wa Kata ya Sakwe, Subi Bunzali amesema kuwa kabla ya Mradi huo, wananchi walikuwa wanapata shida ya Maji na baada ya Mradi huo kukamilika wananchi wamehamasika sababu ukiisha tutapunguza adha ya Maji na kuondoa matumizi ya Maji machafu.
Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Eva Ndegeleki ameipongeza serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kutoa fedha za miradi ya Maji pamoja na RUWASA kwa Usimamizi wao.
Ameitaka Wakala hiyo kuelimisha kuelimisha vijana juu ya Umuhimu wa kutunza miundombinu ya Maji, ili miradi ya Maji iweze kudumu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Kenan Kihongosi ameipongeza serikali kwa kutekeleza miradi ya Maji ambayo imewatua akina mama ndoo za Maji kichwani.
Mwisho.
Post a Comment