MrJazsohanisharma

WANANCHI 4000 WAPIGWA JEKI UJENZI WA ZAHANATI.


 Wananchi waliofika kuwasikiliza wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Simiyu waliotembelea zanahati ya kijiji cha Mwamihanza.


Na Samwel Mwanga, Maswa.


ZAIDI ya wakazi 4,000 wa kijiji cha Mwamihanza wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wameondokana na changamoto ya kutembea umbali wa kilomita nane kufuata huduma ya afya baada ya Mfuko wa hifadhi ya jamii(Tasaf)kuwajengea zahanati kwa gharama ya Sh 129.2 milioni.


Kabla ya ujenzi wa zahanati hiyo,wanakijiji hao walienda kutibiwa katika zahanati za kijiji cha Isanga,Ilamata na Isulilo umbali wa zaidi ya kilomita nane.


Wakizungumza leo Aprili 11,2025 mbele ya wajumbe wa kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)mkoa huo waliotembelea zahanati hiyo,wananchi hao wameishukuru serikali wakidai zahanati iliyojengwa imeepusha vifo vitokanavyo na kuchelewa kupata huduma za afya.


“Kwa kweli zahanati hii itatusaidia sana hivyo jukumu letu  ni kuitunza miundombinu yake ili iweze kudumu kwa muda mrefu,kizazi na kizazi kikute huduma hizi zikiendelea,”amesema Peter Lushu mkazi wa kijiji hicho.


Naye Esther Medard mkazi wa kijiji hicho amesema kuwa  mfuko wa  Tasaf umekuwa msaada kwa wananchi akidai kuwa awali wajawazito walipata shida ya kupata huduma,hali ambayo ilisababisha wengi wao kujifungulia njiani na wengine kupoteza watoto.


“Kutokana na huduma wazazotoa kwa jamii na sisi tumehaidi kutoa ushirikiano,pale ambapo miradi inatekelezwa kupitia mfuko huo tunashiriki kutoa sehemu ya nguvu zetu ili tuwe sehemu ya mradi unaotekelezwa,”amesema.


Emanuel Silanga ni mjumbe wa halmashauri Kuu CCM Taifa kupitia mkoa wa Simiyu anasema kuwa malengo ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na chama hicho imelenga kuhakikisha inawafikishia huduma za afya wananchi kwa kujenga zahanati katika vijiji vyote na vituo vya afya katika kila Kata hapa nchini.


“Hii zahanati iliyojengwa katika kijiji hiki ni sehemu ya mikakati ya serikali inayoongozwa na CCM kuhakikisha kila kijiji kina zahanati na kila kata ina kituo cha afya ili wananchi wasitembee umbali mrefu kufuata huduma za afya,”amesema.


Awali mratibu wa Tasaf wilaya ya Maswa,Grace Tungaraza akisoma taarifa fupi juu ya ujenzi wa zahanati hiyo amesema kuwa fedha hizo zilipatikana kutoka nchi zinazozalisha mafuta Duniani(Opec IV)kupitia miradi ya kupunguza umasikini.

Amesema licha ya kujenga zahanati hiyo pia wameweza kujenga nyumba ya mganga,kichomea taka,choo,ununuzi wa samani na vifaa tiba.


“Niwaombe wananchi wa kijiji hiki pamoja na watumishi wa zahanati hii kutunza vifaa tiba vilivyopelekwa katika zahanati hiyo pamoja na kutunza miundo mbinu ya majengo yaliyopo,”amesema.


MWISHO.


Wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Simiyu wakijadilia jambo mara baada ya kukagua ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mwamihanza.


Jengo la zahanati iliyojengwa katika kijiji cha Mwamihanza wilaya ya Maswa.


Sehemu ya mbele ya jengo la zahanati iliyojengwa katika kijiji cha Mwamihanza wilaya ya Maswa.



Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post