. Viongozi mbalimbali Maswa watoa wito.
Na Samwel Mwanga, Maswa
MKUU wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano amewataka viongozi wa dini kutumia nafasi yao kuhakikisha amani na utulivu wa nchi unaendelea kudumishwa, hasa katika kipindi hiki kinapoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 wa Rais,wabunge na madiwani.
Akizungumza Mei 19, 2025 mjini Maswa katika hafla ya dua ya kuliombea taifa na kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wilayani humo, Dkt. Naano amesema kuwa viongozi wa dini wana nafasi ya kipekee katika kuhamasisha maadili mema na mshikamano wa kitaifa.
"Tunapofanya dua na maombi haya huu si uchawa bali ni jambo muhimu sana. Taifa linahitaji maombi, Rais anahitaji maombi kwa kazi kubwa anayofanya ya kulihudumia taifa letu katika nyanja mbalimbali, nchi hii ni kubwa, hivyo tunafanya jambo jema," amesema.
Ameongeza kusema kuwa amani na utulivu ni nguzo muhimu za maendeleo ya kiuchumi kwa jamii na taifa kwa ujumla, na kuwataka viongozi wa dini wasijikite tu katika mafundisho ya kiroho bali pia wawafundishe waumini wao kuhusu masuala ya kiuchumi.
"Sasa ni wakati wa viongozi wa dini kubadili mtazamo wa baadhi ya waumini wanaoshinda vijiweni kwa kucheza bao, pool table na karata, kwa wilaya hii zipo fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinahitaji kushikwa kwa vitendo," amesema.
Dkt. Naano pia alibainisha kuwa licha ya changamoto ndogo ndogo, serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya majadiliano na ushirikiano kama njia ya kudumisha amani na utulivu.
“Fursa ya majadiliano ni muhimu sana katika jambo la amani na utulivu,maendeleo ni hatua na sisi serikali bado hatujamaliza changamoto zote,tujadiliane ili kumaliza hizo changamoto na ndiyo maana Rais Samia kwa kuona umuhimu huo akaanzisha 4R,”amesema.
Aidha amevitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinatumika vizuri kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu kwa kueleza yale mazuri yote yaliyofanyika na yenye kasoro yaonyeshwe ili yaweze kufanyiwa kazi kwa kushirikiana kwani sote tunajenga nyumba moja ambayo ni Tanzania.
Kwa upande wake, Sheikh wa Wilaya ya Maswa, Isa Eliasa , amesema kuwa ni muhimu kuhakikisha uchaguzi mkuu unakuwa huru na wa haki kwa kuzuia vitendo vya rushwa vinavyoweza kuibua migogoro.
"Rushwa kwenye uchaguzi huvuruga amani na utulivu,ni wajibu wetu kama viongozi wa dini kuikemea kwa nguvu zote," amesema.
Katibu wa Baraza la Amani wilaya ya Maswa, Maulid Mlete ambaye pia ni Katibu wa BAKWATA wilayani humo, alisisitiza umuhimu wa kulinda tunu za taifa na kuwataka waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kusema ukweli kwa jamii bila upotoshaji.
“Waandishi ninyi ni watu muhimu sana katika jamii yetu katika kulinda amani na utulivu wan chi yetu hasa katika kuelekea hiki kipindi cha uchaguzi mkuu hivyo niwaombeni sana kwa kutumia vyombo vyenu mkaiseme kweli ndani ya wilaya hii na mkoa wetu na taifa kwa ujumla,”amesema.
Naye Askofu Raphael Makwale, mwakilishi wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo wilayani humo, alihimiza matumizi ya madhabahu kuhubiri amani, upendo na mshikamano.
"Ni wajibu wetu kama viongozi wa kiroho kuwaelekeza waumini kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuleta vurugu na migawanyiko hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu," amesema.
Mwakilishi wa Jumuiya ya Maridhiano wilaya ya Maswa, Lumaza Chuma, amesema kuwa wao wanatekeleza majukumu yao ya kuhakikisha kuwepo kwa maelewano kati ya pande zinazokinzana katika madhehebu ya dini na jamii, ikiwa ni pamoja na serikali sambamba na kutoa elimu kwa njia ya mikutano ya hadhara kwa kuhubiri masuala ya amani na utulivu hasa kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, alisisitiza umuhimu wa upendo miongoni mwa jamii yote.
"Nimefurahishwa na msemo wa Amani na Upendo,ambapo yalikuwa yananikumbusha sisi waumini wa Kristo katika Biblia ukisoma Mathayo 22 ule mstari 34 hadi 40 unaeleza hayo mambo ya upendo,Mafarisayo walikuwa wanamuuliza Bwana Yesu kuwa katika amri tulizopewa kuna amri kuu ambayo tunapaswa tuitekeleze?,”
“Hivi ni amri kubwa ni ipi tuitekeleze,Bwana Yesu akawajibu mpenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote,na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote,hii ndiyo amri iliyo kuu ya kwanza na ya pili yafanana nayo ni hii mpende jirani yako kama nafsi yako,”amesema.
Amesema kuwa hivyo upendo ndiyo amri kuu kuliko zote licha ya kupewa amri kumi na mwenyezi Mungu kwa hiyo tunapozungumzia masuala ya amani, usalama,ushirikiano na msingi wake ni upendo na tusipokuwa na masuala haya tunaweza kuwa na machafuko na tukiwa na upendo hata kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao tutakuwa na umoja hata kama tuna tofauti za kiitikadi.
MWISHO.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa akizungumza katika mkutano wa viongozi wa dini wilaya ya Maswa.
Shekhe wa wilaya ya Maswa,Issa  Elias akizungumza katika mkutano wa viongozi wa dini kabla ya kuliombea Taifa na kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu.
Viongozi wa madhebu mbalimbali ya dini wilaya ya Maswa wakiwa kwenye mkutano wao wa pamoja wa kuliombea Taifa.



إرسال تعليق