RC SIMIYU AZINDUA KITABU CHA TAKA ZA KIELEKTRONIKI: FURSA KIUCHUMI TZ.

 

Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Simiyu na wilaya ya Maswa kila mmoja akiwa ameshika kitabu cha Taka za kielektroniki fursa kiuchumi Tanzania mara baada ya kitabu hicho kuzinduliwa.


Samwel Mwanga, Maswa.


MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi, ameongoza hafla ya uzinduzi wa kitabu kipya kinachohusu taka za kielektroniki, akikitaja kama chombo muhimu cha kukuza uelewa na kuibua fursa mpya za kiuchumi kwa vijana na jamii kwa ujumla nchini Tanzania.


Kitabu hicho, kilichopewa jina “Taka za Kielektroniki: Fursa  Kiuchumi Tanzania”, ni kwa ajili ya kuongeza uelewa juu ya uwepowa taka hizo kutokana na ongezeko la matumizi ya Tehama nchini kama vile simu, kompyuta, runinga na vifaa vingine vya umeme vilivyotupwa.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Mei 10 mwaka huu mjini Maswa katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo amesema kuwa taka hizo ambazo mara nyingi huonekana kama mzigo, zinaweza kubadilishwa kuwa bidhaa zenye thamani endapo zitatazamwa kwa mtazamo wa kibiashara na kimazingira.


Amesema kuwa kupitia kitabu hicho vijana wa mkoa huo watapata maarifa mengi na kufahamu juu ya taka hizo zinazoweza kubadilishwa na kuwa fursa kwao kwa kujipatia ajira.


“Nitumie fursa hii kumpongeza, Ben Kapela ambaye ni mtumishi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa kwa ubunifu wake huu wa kuona kuna haja ya kuondoa taka katika mazingira yetu kwa kutumia mifumo ambayo itasaidia kutengeneza ajira kwa vijana wetu ndani ya Maswa,ndani ya simiyu na Taifa kwa ujumla,”


“Ni tumie fursa hii kwa vijana wetu katika mkoa wa Simiyu kupata maarifa mengi kupitia kitabu hiki,tembea katika maeneo mbalimbali fundisha watu kwa namna gani hizi taka zinaweza kuleta ajira katika mazingira wanayoishi,”amesema.


Amesema serikali ya mkoa hiyo iko tayari kumsaidia iwapo atahitaji kwenda mbali zaidi ikiwa ni pamoja na kuonana na viongozi wa ngazi za juu za kitaifa na hata katika taasisi za serikali zinazojihusisha na masuala ya mazingira kwa jambo hilo ni mara ya kwanza kufanyika katika wilaya hiyo na mkoa huo kwa ujumla.


“Sisi kama viongozi wa mkoa tunaona fahari kuwa watu wenye maarifa makubwa,wana ubunifu mkubwa,lakini pia jitihada za serikali zimemsaidia kujifunza nje ya nchi,kwa sababu serikali ilifungua milango na akapata fursa ya kwenda kijifunza katika vyuo mbalimbali huko nje ya nchi yetu,hivyo ameuleta ujuzi ndani ya nchi hivyo tunaamini,atarithisha na watu wengine yale maarifa yatakwenda kuleta tija kwa kupunguza takataka hizo na kuongeza ajira kwa vijana,”amesema.


Mwandishi mkuu wa kitabu hicho, Ben Kapela ambaye ni Kaimu Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa taka na usafi katika halmashauri ya wilaya hiyo amesema kuwa lengo la kitabu ni kuwaelimisha wananchi kuhusu namna salama ya kukusanya, kuchambua na kuuza sehemu mbalimbali za taka hizo, ikiwemo metali adimu kama dhahabu, fedha na shaba.


“Vifaa vingi vya kielektroniki vinapomaliza muda wake huko majumbani huwa tuavitupa,badala yake sasa unaweza kuvikusanya, vikavunjwavunjwa na kuzirejesha taka hizo katika hali ambayo utapata malighafi yatakayopelekwa sokoni kwa matumizi ya viwanda vya kutengeneza bidhaa mpya nyingine,”amesema.


Anitha Mboje ni mkazi wa mji wa Maswa amesema kuwa kumekuwa na uingizaji mkubwa wa vifaa vya kielekroniki hapa nchini na mara baada ya matumizi yake kuisha vimekuwa chukizo na madhara kimazingira na kiafya hivyo kugeuzwa kuwa fursa ni habari nje kwa vijana.


 “ Taka za kielektroniki siyo tatizo tu la kimazingira na kiafya kwa sasa bali ni fursa ya kiuchumi, tunahitaji kuhamasishwa  sisi vijana wetu kuingia kwenye sekta hii ambayo bado haijachangamkiwa vya kutosha,” amesema.


Naye BoaziMasunga mwananchi wa kijiji cha Sayusayu wilayani humo amesema kuwa elimu hiyo inapaswa kutolewa kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya vijana na wanawake ili waweze kujiajiri kwa kujipatia kipato.


“Haya makundi mawili katika jamii ambayo ni vijana na wanawake yanapaswa kupatiwa hii elimu ambayo imekuja kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa ukubwa wa taka za kielekroniki katika jamii yetu,hivyo zikigeuzwa kuwa fursa zitasaidia watu kujipatia ajira,”amesema.


Pia amesisitiza kuwa kwa sasa ipo haja ya kuingiza elimu kuhusu taka za kielektroniki katika mitaala ya shule na vyuo, ili kuandaa kizazi chenye ujuzi na uelewa wa fursa mpya za kiuchumi.


Kwa mujibu wa mwandaaji wa kitabu hicho,taarifa ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa kuhusu taka za kielektroniki ya mwaka 2019 inaonyesha ongezeko kubwa zaidi la taka hizo ambapo kuanzia mwaka 1998 hadi 2008 wastani wa taka za kielekroniki kwa mwaka ni tani 1.37 wakati wastani wa ongezeko la taka hizo kuanzia mwaka 2008 hadi 2017 ni wastani wa tani 2.32 yaani mara mbili ya miaka kumi iliyopita.


MWISHO.


Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi (kushoto) akimkabidhi, Maisha Mtipa (kulia) ambaye ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, kitabu cha Taka za kielektroniki fursa kiuchumi Tanzania mara baada ya kitabu hicho kuzinduliwa.


Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi(kulia)akiwa na Ben Kapela (kushoto) wakiwa waneshilikia kitabu cha Taka za kielektroniki fursa kiuchumi Tanzania mara baada ya kitabu hicho kuzinduliwa.


Ben Kapela ambaye ni Mwandishi wa kitabu cha Taka za kielektroniki fursa kiuchumi Tanzania akizunguza kabla ya uzinduzi wa kitabu hicho.





Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post