TAKUKURU Simiyu yaokoa miradi ya Bilioni 6 isijengwe chini ya kiwango.

 

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Simiyu Manyama Tungaraza, akizungumza na waandishi wa Habari Jana (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025. (Picha na Derick Milton)

Ofisi za Takukuru Mkoa wa Simiyu.


Na Derick Milton, Bariadi.


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Simiyu, imefanikiwa kuokoa kiasi cha zaidi ya Sh Bilioni 6 ambazo zilitolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya elimu katika mkoa huo ambayo utekelezaji wake ulibainika kujengwa chini ya kiwango.


Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Takukuru Mkoa Manyama Tungaraza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa waandishi wa Habari katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025.


Alisema kuwa miradi hiyo ni ujenzi wa shule ya Sekondari ya Wavulana ya Simiyu ambayo ujenzi wake unagharimu Sh Bilioni 4.1, Ujenzi wa Shule ya Sekondari Kabondo ulioko katika Wilaya ya Meatu ambao unagharimu Sh Milioni 584,000,000.


Mradi mwingine ni ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Amali ambao unatekelezwa katika kata ya Mwamapalala Wilayani Itilima ambao unagharimu kiasi cha Sh Bilioni 1.6.


Alisema kuwa katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wavulana ya Simiyu, walibaini uwepo wa baadhi ya miundombinu yake yakiwemo madarasa kujengwa juu ya bomba la maji safi pamoja na utekelezaji wake kuchelewa kwa siku 119.


“ Baada ya kubaini jambo hilo tulizishirikisha mamlaka husika, ambapo Bomba hilo liliondolewa maana hiyo ilikuwa hatari kubwa kwa miundombinu hiyo kama bomba lingelipasuka, lakini muda wa ujenzi nao uliongezwa na mradi unaendelea kutekelezwa kwa kasi na utakamilika Julai 18, 2025,” alisema Tungaraza.


Katika mradi wa Ujenzi wa Shule ya Sekondari Kabondo ulioko katika Wilaya ya Meatu Mkuu huyo wa Takukuru alisema kuwa walibaini kuwa fundi ambaye alishinda tenda ya ujenzi ambapo mkataba wake ulitamka akamilishe kazi hiyo ndani ya siku 90.


“ Tangu fundi huyo apewe kazi na hadi kufikia tarehe ya ukomo wa mkataba fundi huyo alikuwa ametekeleza mradi huo kwa asilimia 10 tu, na tulibaini alikuwa na uwezo mdogo wa kifedha, tulifanya kikao na wahusika wa mradi akatafutiwa fundi mwingine mwenye uwezo na mradi umekamika,” alisema Tungaraza.


Katika mradi wa tatu wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Amali katika Wilaya ya Itilima, Takukuru ilibaini uwepo wa ucheleweshwaji mkubwa wa vifaa vya ujenzi kufika katika eneo la mradi.


Alisema kuwa walifanya vikao na wahusika wa mradi huo na kasoro hizo ziliondolewa ambapo imepelekea kasi ya ujenzi kuongezeka kutoka asilimia 25 ya awali hadi kufikia asilimia 75.


MWISHO.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post