![]() |
| Ofisi za Takukuru Mkoa wa Simiyu. |
Na Derick Milton, Bariadi.
Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Simiyu, imefanikiwa kuokoa kiasi cha
zaidi ya Sh Bilioni 6 ambazo zilitolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza
miradi ya elimu katika mkoa huo ambayo utekelezaji wake ulibainika kujengwa
chini ya kiwango.
Hayo yamesemwa
jana na Mkuu wa Takukuru Mkoa Manyama Tungaraza wakati akitoa taarifa ya
utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa waandishi wa Habari katika kipindi
cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Alisema kuwa
miradi hiyo ni ujenzi wa shule ya Sekondari ya Wavulana ya Simiyu ambayo ujenzi
wake unagharimu Sh Bilioni 4.1, Ujenzi wa Shule ya Sekondari Kabondo ulioko
katika Wilaya ya Meatu ambao unagharimu Sh Milioni 584,000,000.
Mradi mwingine ni
ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Amali ambao unatekelezwa katika kata ya
Mwamapalala Wilayani Itilima ambao unagharimu kiasi cha Sh Bilioni 1.6.
Alisema kuwa
katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wavulana ya Simiyu, walibaini
uwepo wa baadhi ya miundombinu yake yakiwemo madarasa kujengwa juu ya bomba la
maji safi pamoja na utekelezaji wake kuchelewa kwa siku 119.
“ Baada ya kubaini
jambo hilo tulizishirikisha mamlaka husika, ambapo Bomba hilo liliondolewa
maana hiyo ilikuwa hatari kubwa kwa miundombinu hiyo kama bomba lingelipasuka,
lakini muda wa ujenzi nao uliongezwa na mradi unaendelea kutekelezwa kwa kasi
na utakamilika Julai 18, 2025,” alisema Tungaraza.
Katika mradi wa Ujenzi
wa Shule ya Sekondari Kabondo ulioko katika Wilaya ya Meatu Mkuu huyo wa
Takukuru alisema kuwa walibaini kuwa fundi ambaye alishinda tenda ya ujenzi
ambapo mkataba wake ulitamka akamilishe kazi hiyo ndani ya siku 90.
“ Tangu fundi
huyo apewe kazi na hadi kufikia tarehe ya ukomo wa mkataba fundi huyo alikuwa
ametekeleza mradi huo kwa asilimia 10 tu, na tulibaini alikuwa na uwezo mdogo
wa kifedha, tulifanya kikao na wahusika wa mradi akatafutiwa fundi mwingine
mwenye uwezo na mradi umekamika,” alisema Tungaraza.
Katika mradi wa
tatu wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Amali katika Wilaya ya Itilima,
Takukuru ilibaini uwepo wa ucheleweshwaji mkubwa wa vifaa vya ujenzi kufika
katika eneo la mradi.
Alisema kuwa walifanya vikao na wahusika wa mradi huo na kasoro hizo ziliondolewa ambapo imepelekea kasi ya ujenzi kuongezeka kutoka asilimia 25 ya awali hadi kufikia asilimia 75.
MWISHO.


إرسال تعليق