KATA ZA SAKWE, ITUBUKILO ZANUFAIKA NA MIRADI YA MAENDELEO.

MBUNGE wa Jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo Mathew akiongea kwenye Mkutano maalumu wa kuwasilisha Ilani ya CCM (2020/2025) uliofanyika kata ya Itubukilo.



Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.


MBUNGE wa Jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo Mathew amemshukuru Rais Dk. Samia Suluh Hassan kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo ambayo imechochea ukuaji wa uchumi katika kata za Itubukilo na Sakwe wilayani Bariadi. 


Akizungumza na wanachama wa CCM leo katika mikutano ya kuwasilisha Ilani (2020/2025) iliyofanyika kwenye kata hizo, Mhandisi Kundo amesema katika miaka minne ya Rais Dk. Samia wananchi wamefikiwa na huduma za umeme, barabara na maji tofauti na ilivyokuwa awali. 


Amesema kabla ya uongozi wa Rais Dk. Samia, kata hizo zilikuwa kisiwani kutokana na ukosefu wa umeme na barabara, lakini sasa vijiji vya Pugu, Utubukilo, Sakwe, Mwanzoya, Mwambalange, na Mwangimu vimefikiwa na Umeme na wananchi wameanza kunufaika.


"Vijiji vyenu vilikuwa kisiwani, hapakuwa na umeme wala barabara zilikuwa hazipitiki lakini leo kuna Umeme, Barabara na Maji...ndani ya miaka minne kata ya Sakwe mmepokea shilingi Mil. 245 za Barabara na shilingi Mil. 350 kujenga mnara wa mawasiliano" amesema.


Mhandisi Kundo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji ameongeza kuwa katika kata ya Sakwe kwa miaka mitano (2015/2020) ilipokea shilingi Mil. 321, huku miaka mitano (2020/2025) kata hiyo imepokea shilingi Bil. 1.516 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.


Katika Kata ya Itubukilo, Mhandisi Kundo amesema kwa miaka mitano (2020/2025) serikali ya Dk. Samia imetoka kiasi cha shillingi 409 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa barabara ambao umefungua na kurahisisha usafiri na usafirishaji.


"Tunatambua barabara zimeharibika kutokana na mvua zilizonyesha, lakini tunaamini serikali ni sikivu itarekebisha...tumeleta pampu za maji ili kuboresha upatikanaji wa huduma za maji, pia bajeti ijayo tutafikisha umeme kwenye vitongoji" amesema Mhandisi Kundo.


Akiwa kata ya Itubukilo, Mhandisi Kundo amekabidhi mipira 23 na jezi pea 6 ambapo vijiji vya Mwangumu, Pugu, Itubukilo, Mwambalange na Kihalahala vimekabidhiwa mipira minne na jezi pea Moja huku kata ya Itubukilo ikipewa jezi 1 na mipira mitatu pamoja na pampu mojamoja ya maji.



Kwenye kata ya Sakwe, Mbunge huyo amekabidhi mipira 15 kwa ajili ya vijiji vya sakwe, Mwangimu na Itubukilo ambapo kila Kijiji kimepata mipira minne na jezi pea 1 huku kata ikipewa mipira mitatu na jezi pea Moja pamoja na pampu Moja Moja ya maji. 


Mwisho.
















Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم