- DC Dkt Naano aagiza oparesheni kabambe.
Na Samwel Mwanga, Maswa
SERIKALI ya Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, imetangaza oparesheni maalum ya kuwakamata wafanyabiashara wote wanaotoa mikopo kwa wananchi bila kusajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT), wakituhumiwa kuwaumiza wananchi kwa riba kubwa na mikataba ya ujanja.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano, alitoa tamko hilo leo Ijumaa, Mei 13, 2025, mjini Maswa wakati akikabidhi mikopo ya Shilingi milioni 133.6 kwa vikundi vya uzalishaji mali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Wafanyabiashara hawa siyo tu wanatoza riba kubwa, bali wanatengeneza mikataba ya kijanja kwa nia ya kuwadhulumu wananchi iwapo kesi itafika mahakamani. Oparesheni ya kuwakamata inaanza mara moja. Tunawafahamu na tutawapeleka kwenye vyombo vya sheria,” amesema Dkt. Naano kwa msisitizo.
Aidha, ameeleza kuwa mikopo inayotolewa na Halmashauri kupitia mapato ya ndani haina riba na ni heshima ya serikali kwa wananchi wake, akisisitiza umuhimu wa kurejesha fedha kwa wakati ili kuwanufaisha wengine.
Miongoni mwa walionufaika ni Lushinge Salina, mlemavu kutoka kijiji cha Sola, aliyepokea mkopo wa Bajaji na kusema: “Ninaishukuru Serikali kwa kutukumbuka watu wa makundi maalum. Nitaitumia Bajaji kujipatia kipato.”
Elizabeth Paul kutoka kijiji cha Mwamitumai, amesema: “Mkopo huu utanisaidia kuongeza mtaji. Nitaachana kabisa na mikopo ya mitaani maarufu kama ‘Kausha damu’.”
Vijana nao hawakubaki nyuma. Marco Paul wa kijiji cha Sengwa amesema mkopo huo utawasaidia kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Maswa, Paul Maige, aliwataka wanufaika kutumia fedha hizo kama kichocheo cha maendeleo kwao na kwa wilaya kwa ujumla.
Akitoa taarifa ya ugawaji mikopo hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii, Lucia Misinzo, amesema kuwa ni awamu ya pili kwa makundi maalum. Vikundi tisa vya wanawake vilipata Sh milioni 78, vijana vikundi vinne Sh milioni 36 na vikundi vitatu vya watu wenye ulemavu Sh milioni 19.
Hata hivyo, amesema changamoto zimebaki ikiwemo uchache wa fedha kulinganisha na mahitaji pamoja na uelewa mdogo wa baadhi ya wanakikundi kuhusu matumizi ya mfumo wa mikopo ya asilimia 10.
MWISHO.




إرسال تعليق