RAIS DK. SAMIA AZINDUA OFISI ZA TRA, ATAKA UWAJIBIKAJI.




Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amezindua Jengo la Ofisi za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), katika Mkoa kikodi Simiyu ambalo limejengwa kwa gharama ya shilingi Bil. 9.4 huku akiwataka watumishi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa weledi.


Aidha, Rais Samia amewataka Wananchi kujenga Utamaduni wa Kulipa kodi kwa Maendeleo ya Taifa ili kujenga Uchumi imara na kwamba wasipolipa Kodi Taifa litaendelea kubakia la watumwa.


Akizungumza leo mara baada ya uzinduzi wa Majengo ya Ofisi za TRA nchini, Rais Samia ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kukusanya Kodi jambo ambalo limeifanya serikali kupata pesa za kuendesha miradi pamoja na kuboresha maisha ya watumishi na kurahisisha utoaji wa huduma.


"Mamlaka ya Mapato nchini, twendeni tukakusanye kodi kirafiki, nilikwambia Yusuph, mfanyabiashara awe rafiki yako na siyo adui wako...Ile kufunga Biashara na akaunti za watu siyo nzuri,  kuna wengine masugu tutafanya hivyo, lakini tuwaite na kuwaelimisha ili tukusanye pesa yetu ya ndani" amesema.


Alisema  nchi lazima ikusanye kodi za ndani na kwamba hakuna nchi inayoendeshwa bila pesa za walipa Kodi na kusisitiza kuwa nchi ya Tanzania imebairikiwa  kupata Madini, Bahari, Maziwa, Ardhi nzuri hivyo tunasubiri mtu aje achimbe na atupe kidogo, na sisi kama serikali lazima tukusanye, tuendeshe nchi yetu vizuri.


"Niwapongeze Wakandarasi, Majengo haya yameboresha Utendaji kazi hakuna sababu ya kushindwa kufanya kazi, ndani kuna mifumo inayowapa urahisi wa kufanya kazi zenj...Juzi nimethibitisha wafanyakazi zaidi ya 1800 waajiriwe ili kuongeza Jeshi la TRA na pia tumewaongezea kiwango cha makusanyo katika bajeti hii na Sina wasiwasi mnaweza kufikia" amesema.


Rais Samia ameeleza kuwa toka aingie madarakani, Mamlaka hiyo imekuwa ikiongeza ukusanyaji wa mapato ambao umepanda na kufikia asilimia 98 mpaka 99 huku wakitarajia kuwenda mbele zaidi ili kufikia Malengo waliyojiwekea.


Amesema kupitia ukusanyaji wa Mapato, serikali imefanikiwa kujenga vituo vya afya ambavyo vinatoa huduma ya matibabu ya kisasa, huduma za Umeme zimefika kwa kila mahali ili kuwezesha wananchi wazalishe na kuchangia mapato kupitia Kodi.


"TRA jitahidini kukusanya mapato kwa njia rafiki, lakini siyo kubembelezana, Majengo haya kuna kila raha, majengo mazuri yasiwapandishe mabega, shukeni kutoa huduma kwa wanachi, kusanyeni Kodi yetu Kwa maslahi ya Taifa letu" amesema.


Akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa.Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Stanslau nyongo ameipongeaza serikali kwa kujenga Jengo hilo ambalo litarahisisha utoaji wa huduma za kikodi.


Nyongo amesema kuwa Walipa Kodi katika Mkoa wa Simiyu wanamshukuru kupata Jengo la kutolea huduma na kwamba wanaona namna fedha zao zinatumika ipasavyo.


Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa Jengo hilo, Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Yusuph Mwenda amesema Mkoa wa kikodi Simiyu ni moja ya mikoa ya kikodi 33 nchini na kwamba ujenzi wa Jengo la Ofisi za TRA Mkoa huo ulianza mwaka 2023,


"Ujenzi wa Jengo hili ulianza mwaka 2023 na limemalizika mwaka huu, Jengo lina ghorofa tatu na lina uwezo wa kuchukua watumishi 200...Jengo ni la kisasa na limegharimu kiasi cha Shilingi Bil. 9.4 pia hili Jengo ni mojawapo ya majengo yaliyogharimu shilingi Bil. 116 yanayoendelea kujengwa katika mikoa 33 nchini" amesema Kamishina huyo.


Amesema kuwa kukamilika kwa Jengo hilo kutarahishisha utoaji wa huduma bora kwa walipa Kodi Mkoani Simiyu ambao wanafika na Kulipa kodi, pia litatumika kuelimisha walipa Kodi na watumishi watapata nafasi nzuri ya kutoa huduma bora kwa wateja.


Alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Mkoa wa Simiyu uliweka Malengo ya kukusanya shilingi Bil. 22, lakini mpaka sasa wamefanikiwa kukusanya shilingi Bil. 25 kutokana na wananchi kuhamasika kutokana na kuwepo kwa majengo ya kisasa ambayo yanajengwa nchi nzima.


Aliongeza kuwa kuanzia mwezi Julai 2024 mpaka mwezi Agost, Mamlaka ya Mapato Tanzania Bara na Visiwani walipaswa kukusanya shilingi Tri 27, lakini mpaka mwisho wa mwezi May, wamefanikiwa kukusanya shilingi  Trioni 28.61.


Kamishna hiyo alimwahidi Rais Dk. Samia kuwa kutokana na Uwekezaji wa Majengo, vifaa na watumishi, watafanya kazi nzuri ya kukusanya Kodi kwa mujibu wa Sheria inavyotakiwa.


Mwisho.








Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post