|  | 
| Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa Ofisi za TRA Mkoa wa Simiyu. | 
Na Frank Kasamwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan, amewahimiza wafanyabiashara kuendeleza utamaduni wa kulipa kodi
ili kuiwezesha serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kupunguza
utegemezi wa mikopo ya nje.
Amesema
kuwa masharti ya mikopo kutoka nje yameendelea kuongezeka siku hadi siku, hivyo
ni muhimu kwa nchi kuimarisha uwezo wa kukusanya mapato ya ndani ili iweze
kujitegemea.
Rais
Dkt. Samia alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa ofisi za Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu. Amesisitiza kuwa hakuna nchi yoyote
duniani inayoweza kujiendesha bila mapato ya kodi.
Ameeleza
kuwa ili wananchi waweze kupata huduma bora za kijamii kama maji safi, huduma
za afya, umeme na nyinginezo, ni lazima serikali iwe na mapato madhubuti ya
ndani, na kila mtu anayestahili kulipa kodi atimize wajibu huo.
"Wananchi wenzangu na wafanyabiashara, wale wanaotukopesha fedha
wanaweza kufanya hivyo kwa sababu raia wao wanalipa kodi. Sasa ni mpaka lini tutaendelea
kukopa? Hatuhitaji kuendelea kukopa lazima tukusanye kodi zetu wenyewe," alisema Rais Samia.
Katika
hatua nyingine, Rais amewataka maafisa wa TRA kukusanya kodi kwa njia rafiki na
ya ushirikiano badala ya kutumia nguvu au vitisho.
Amesema
kuwa watumishi wa TRA wanapaswa kuzingatia mbinu za kiungwana, kama vile
kufanya mazungumzo na wafanyabiashara ambao bado hawajalipa kodi na kukubaliana
nao juu ya namna ya kulipa kwa awamu.
"Njia ya kwanza ya kukusanya kodi iwe ni ya kirafiki. Kwa wale ambao
hawajalipa, waiteni, fanyeni nao kikao, kubalianeni namna ya kulipa kidogo
kidogo ili serikali isipoteze mapato kabisa," alisisitiza.
Rais
Samia ameongeza kuwa matumizi ya nguvu katika ukusanyaji wa kodi kama vile
kuchukua vifaa vya biashara, nyaraka au kufungia akaunti za benki visiwe chaguo
la kwanza, bali litumike pale tu wafanyabiashara wanapokaidi kwa makusudi.
"Matumizi ya nguvu kama kuchukua kompyuta ya mfanyabiashara, vitabu
vyake, au kufungia akaunti zake visianze kutumika moja kwa moja. Bali vitumike
tu pale mtu anapokaidi makusudi," alisema Rais Dkt. Samia.
Hata
hivyo, Rais Samia pia amewataka wafanyakazi wa TRA kufanya kazi kwa weledi na
kuhakikisha wanatimiza malengo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Amebainisha
kuwa serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi
wa TRA, ikiwa ni pamoja na kupitisha ajira mpya takribani 1,800 ndani ya
mamlaka hiyo.
إرسال تعليق