
Na Samwel Mwanga, Maswa
WAKULIMA wa zao la pamba katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, wameeleza kuridhishwa na matumizi ya mizani ya kidigitali katika ununuzi wa zao hilo msimu huu.
Wakizungumza Juni 5 2025 wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) katika vijiji vya Nguluguli na Mwamanenge wilayani humo ambayo ilitoa fursa kwa viongozi hao kujionea hali halisi ya uvunaji na ununuzi wa zao hilonna kusikiliza kilio cha wakulima wa zao hilo moja kwa moja.
Shija Emanuel ni mkulima katika kijiji cha Nguliguli amesema kuwa licha ya kupokea kwa furaha mageuzi hayo ya kutumia mizani ya kisasa lakini bado ina chanhamoto ya kuishiwa na chaji mara kwa mara.
“Tunapokea kwa furaha mageuzi haya ya kutumia mizani ya kisasa,hii imesaidia sana kupunguza malalamiko ya upunjwaji hata hivyo, tunakumbana na changamoto ya mizani kuishiwa chaji mara kwa mara,wakulima wengine hulazimika kurudi nyumbani bila kuuza pamba yao,” amesema.
Naye Mary John mkulima wa kijiji cha Mwamanenge amesema kuwa teknolojia hiyo imeondoa malalamiko ya kupunjwa uzito wa mazao yao kama ilivyokuwa ikiripotiwa katika miaka ya nyuma.
“Zamani tuliambiwa uzito tu,hatukujua kama tunaibiwa au la,lakini sasa tunaona kilo zinavyosoma,kinachotatiza ni kwamba mara nyingine mzani haufanyi kazi kwa sababu ya chaji,” amesema.
Martine Mayunga mkulima wa kijiji cha Nguliguli amesema kuwa mara nyingine wanalazimika kusubiri muda mrefu au kurudi siku nyingine kuuza pamba kwa sababu mzani hauwashi hali ambayo inawakatisha tamaa.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba,Agrey Mwanri amesema kuwa bodi hiyo imepokea malalamiko hayo na kuahidi kuwa changamoto hiyo itashughulikiwa kwa haraka.
“Tutashirikiana na wanunuzi pamoja kuhakikisha kuwa vifaa vya kuchaji mizani, kama vile 'power banks'vinapatikana katika kila kituo cha ununuzi kwani tumebaini ya kuwa umeme unaotumia ya nguvu za jua si mkubwa hautoshelezi katika vifaa vyetu,hili ni jambo dogo lakini lina athari kubwa kwa mkulima,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya pamba nchini,Marco Mtunga amewaagiza Maafisa ugani wa BBT kutoruhusu pamba kununuliwa na mkulima atakayeleta pamba chafu arudishwe akaichambue.
MWISHO.

Post a Comment