Wananchi Msiharibu Vyanzo vya Maji; Dkt. Nawanda.


MKUU wa mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda (aliyesimama) akiwahutubia Wananchi waliojitokeza wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji kimkoa yaliyofanyika katika Kijiji Cha Ngulyati Wilaya ya Bariadi.
 
 
  MKUU wa mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda akigawa maji ya kunywa Kwa wananchi waliohudhuria sherehe ya kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Maji yaliyofanyika kimkoa katika Kijiji Cha Ngulyati Wilaya ya Bariadi.

 

MENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani).

 

Bango lililobeba ujumbe wa Wiki ya Maji mwaka huu.


Na Samwel Mwanga, Bariadi.

 

MKUU wa mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda amewataka wananchi kuacha kuvamia na kuharibu vyanzo vya maji isipokuwa wavilinde na kuvitunza.

 

Pia amekemea tabia ya baadhi watu wanaoharibu miundo mbinu ya maji kama vile kukata mabomba ya Maji.

 

Dkt Nawanda amesema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji katika mkoa huo iliyofamyika kwenye Kijiji cha Ngulyati wilayani Bariadi.

 

Amesema serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi katika sekta ya Maji Ili kuhakikisha Wananchi wanapata Maji safi na salama hivyo jukumu la kulinda vyanzo vya Maji ni letu sote.

 

"Kwa mwaka wa fedha uliopita katika mkoa wetu wa Simiyu tulipatiwa kiasi cha Sh Bilioni 35 na serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Maji hivyo hatuna budi kuvilinda vyanzo vya Maji  Ili viwe endelevu,"

 

"Tusiharibu vyanzo vya maji kwa kufanya shughuli za kibinadamu kama vile kulima na kuingiza mifugo tukifanya hivyo tutasababisha kuharibu Mazingira  na kusababisha tusipate maji hivyo ni lazima tuvilinde vyanzo vyetu na watakaokwenda kinyume ni lazima sheria zitumike,"alisema.

 

Dkt Nawanda alionesha kutofurahishwa na tabia ya baadhi ya watu wanaohujumu miundombinu ya Maji na kuliagiza jeshi la polisi katika mkoa huo kuwakamata watu wote watakaobainika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

 

"Rpc hakikisha watu wote wanaohujumu miundombinu ya Maji katika mkoa wetu wa Simiyu watakaobainika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria maana Serikali inatoka fedha nyingi sana kwenye miradi ya Maji kama Mradi huu uliopo hapa kwenye Kijiji Cha Ngulyati,"amesema.

 

Awali Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala amesema kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya Maji Vijijini katika mkoa huo ni asilimia 71.

 

Mhandisi Mariam amesema kuwa mahitaji ya maji kwa watu waishio vijijini katika mkoa huo ni Lita 48,440725 kwa siku ila maji yanayozalishwa kwa siku ni Lita 34,456,000 kwa siku ambayo yanahudumia jumla ya watu 1,378,240 wanaoishi vijijini.

 

Amesema kuwa Ruwasa katika mkoa huo inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishiyo vijijini na kuhakikisha kuwa miradi yote iliyokamilika kujengwa inatunzwa na kutengenezwa kwa kutumia fedha inayotokana na mauzo ya Maji ya eneo husika.

 

Aidha Mhandisi Mariam ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuwapatia fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika mkoa huo.

 

"Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu tunamshukuru sana kwa kutupatia fedha nyingi sisi Ruwasa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na tunamuhaidi hatuwezi kumuangusha tutasimamia fedha hizo Ili tuweze kuhakikisha tunawapatia Maji Wananchi wanaoishi maeneo ya Vijijini,"amesema.

 

Kauli mbiu ya Mwaka huu ya  Maadhimisho ya Wiki ya Maji ni "Kuongeza Kasi ya Mabadiliko katika Sekta ya Maji Kwa Maendeleo Endelevu ya Uchumi".

 

Mwisho.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post