
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WAKULIMA bora sita wa Pamba kutoka Chama Cha Ushirika Itemelo Amcos kilichopo Kijiji cha Isenge kata ya Dutwa wilayani Bariadi Mkoani Simiyu wameipongeza serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuleta Maafisa Ugani wa BBT jambo ambalo limeongeza tija ya uzalishaji huku akiahid kuongeza uzalishaji msimu ujao.
Wamesema kuwa kutokana na elimu waliyopata, umewasaidia kuongeza uzalishaji kutoka kilo 300 kwa ekari moja na kufikia kilo 1000 kwa ekari moja na kwamba baada ya uzalishaji huo wamepewa motisha ya zawadi ya pikipiki kwa kila mmoja.
Wakizungumza za waandishi wa Habari za Pamba, wakulima hao wamesema kuwa wameongeza uzalishaji kutokana na kuzingatia ya Elimu ya Kilimo cha pamba pamoja na matumizi sahihi ya mbolea.
Saimon Malugu ambaye ni mkulima hodari amesema awali alikuwa anazalisha kilo 200 mpaka 300 kwa ekari moja, lakini kutokana na elimu aliyopewa ameongeza uzalishaji na kufikia kilo 1000 katika ekari hiyo hiyo moja.
Naye Masaka Manyangu, mkulima hodari amesema kuwa Maafisa Ugani wa Jenga Kesho Bora (BBT) wametoa Elimu moja kwa moja mashambani jambo ambalo limeomwongezea uzalishaji na kufikia kilo 1200 kwa ekari moja.
"Tunamshukuru Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwa kutoa zawadi za pikipiki baada ya kuongeza uzalishaji...tunaahidi kuwa wakulima bora na wa mfano katika msimu ujao" amesema Manyangu.
Mwenyekiti wa Itemelo Amcos, Juliana Mayenga amesema kuwa motisha ya zawadi ya pikipiki kwa wakulima hao imekuwa hamasa kwao na wakulima wengine watabadilika kwa Vitendo siyo maneno.
Ndinda Anthony, Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Bariadi, anasema Wakulima bora kutoka Itemelo Amcos wameahidi kuzingatia ubora na watafundisha Wakulima wengine kuendelea kuzalisha kwa tija.
Amesema zawadi za Pikpiki zilizotolewa na Waziri Bashe, zimeleta motisha na wengi wameahid kulima kwa kufuata maelekezo ya Maafisa Ugani.
Ndinda, ameongeza kuwa wilaya ya Bariadi inatarajia kuvuna Kilo mil. 36 ambapo mpaka sasa wamevuna kilo mil.6 na ununuzi bado unaendelea ambapo mwaka jana walivuna kilo Mil. 9.
"Elimu ya Kilimo imeongeza uzalishaji kwa kushirikiana na BBT, Dutwa tulisambaza mbolea hai ndio maana tumepata wakulima hodari waliopata tija...Bariadi kuna wakulima wengi waliozingatia kanuni, tunao zaidi ya wakulima 8000 na wengi wamevuna kuanzia kilo 800 kwa ekari moja." Amesema Ndinda.
Mwisho.
إرسال تعليق