WANNE KUMVAA NAIBU WAZIRI NYONGO UBUNGE JIMBO LA MASWA MASHARIKI.


 

Samwel Mwanga,Maswa


NAIBU  Waziri wa Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Stanslaus Nyongo, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wanachama wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojitokeza kutaka kumng’oa katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.


Taarifa iliyotolewa leo, Julai 29, 2025, na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Amos Makala, imeeleza kuwa jumla ya wanachama watano wamepitishwa kuomba ridhaa ya wanachama wa CCM kupeperusha bendera ya chama hicho jimboni humo.


Mbali na Nyongo ambaye anamaliza miaka 10 akiwa mbunge wa jimbo hilo, wengine waliopitishwa ni George Lugomela, Nyangi Kimora, Mayunga George na Adolf Samia.


Nyongo aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2015 na kisha kuchaguliwa tena mwaka 2020. Katika kipindi chake, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Madini kabla ya kuhamishiwa Ofisi ya Rais.


Hatua ya CCM kuidhinisha majina matano inaashiria ushindani mkubwa ndani ya chama, huku macho ya wengi yakielekezwa kwa wanachama watakaoamua nani atakayepeperusha bendera ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao.


Mwisho. 





Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post