Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza na wafugaji katika bando la Maonesho la mifugo la halmashauri ya wilaya ya Maswa katika viwanja vya Nyakabindi mjini Bariadi.
Na Samwel Mwanga, Simiyu
WAFUGAJI kutoka mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga wametakiwa kuachana na ufugaji wa mazoea na kuanza kutumia mbinu za kisasa katika ufugaji ili kukidhi mahitaji makubwa ya soko la mazao ya Mifugo la ndani na nje ya nchi ikiwemo nyama, maziwa na ngozi.
Akizungumza leo Ijumaa, Agosti 8, 2025, kwenye maonyesho ya wakulima Nanenane, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, mara baada ya kutembelea banda la maonesho ya mifugo la halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu katika Maonesho ya kanda ya Ziwa Mashariki yanayofanyika viwanja vya Nyakabindi mjini Bariadi.
Amesema kuwa wafugaji walio wengi hapa nchini bado wanafuga kwa mazoea kuwa na idadi kubwa ya mifugo lakini bado wanashindwa kuihudumia kwa kuipa malisho mazuri na hivyo hawezi kukupa bei nzuri ya nyama kwenye soko.
“Ng’ombe wanaofugwa kwa mazoea hawawezi kukupa bei nzuri sokoni. Tuchague mbegu bora, tuwalishe lishe yenye virutubisho kamili, tuwape chanjo kwa wakati na kuwatunza kitaalamu. Hapo ndipo tutaona faida ya kweli ya ufugaji,” amesema.
Akibainisha umuhimu wa mabadiliko hayo amesema kuwa masoko ya nchi jirani na yale ya Mashariki ya Kati yana uhitaji mkubwa wa nyama bora, lakini wafugaji wengi bado hawajafikia viwango vinavyohitajika kimataifa.
Shigile Nkonya mfugaji kutoka kijiji cha Gulla wilaya ya Maswa amesema kuwa anafuga ng’ombe aina ya Simental kisasa ambaye kwa sasa ana umri miaka mitatu na uzito wa kilogram 930.
“Huyu ng’ombe ninayemfuga kisasa ni dume na nina mchunga kawaida ila namuandalia malisho yaliyo bora ili kuweza kupata mazao bora ya ng’ombe ambayo ni pamoja na maziwa na nyama,”amesema.
Naye Yusuph Ndamo mfugaji kutoka kijiji cha Lalago wilaya ya Maswa amesema kuwa anafuga ng’ombe dumea aina ya Boran kwa ajili ya kupandisha ili kupata mbegu bora kwa ajili ya kupata nyama na maziwa yaliyo bora yanayokidhi viwango katika soko.
“Huyu ng’ombe niliye naye nimatumia kupandisha kwa ajili ya kupata mbegu bora na kwa sasa nina ndama 16 ambao wanatokana na aina hii ya ng’ombe ambayo ni Boran na mfugaji anapokuja kwa ajili ya kupandisha tu,"
"Huduma ya kupandisha ni bure na lengo tuweze kupata maziwa na nyama iliyo bora kwa ustawi wa jamii yetu pamoja na kuhimili soko kulinganisha na wafugaji kutoka nchi jirani na tangu nianze kumfuga gharama yake ni ya kawaida na kwa sasa ni miaka mitatu na anauzito wa kilogram 900,”amesema.
Robert Maduhu ni mfugaji kutoka wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu aliyetembelea banda hilo amesema kuwa changamoto kubwa wafugaji walio wengi katika mkoa huo ni ukosefu wa mitaji na elimu ya kitaalamu ya ufugaji wa kisasa.
“Tunataka kufuga kisasa kama tunavyosikia, lakini changamoto ni gharama za lishe na huduma za mifugo. Tunaomba serikali itusaidie mitaji na masoko yenye uhakika,” amesema.
Daktari wa Mifugo halmashauri ya wilaya ya Maswa,Charles Musira amesema kuwa amesema kuwa ng’ombe hao wamekuwa wakienda kuchunga na kurudi na wameandaliwa kwa ajili ya kuboresha ngombe wa asili kwa kupandisha ili waweze kupata ambao watakuwa na mazao bora.
“Hawa ng’ombe wanakuwa kwa kasi na kwa muda mfupi sana na ndani ya miaka miwili au mitatu anakuwa ameshapevuka na anaweza kuishi katika mazingira yoyote yale ni mzuri kwa ajili ya nyama na maziwa na hawashambuliwi ma magonjwa hovyo hovyo kutokana na kuyazoea mazingira yetu na wako kwa ajili ya kupandisha katika ng’ombe wetu wa asili,”amesema.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Mashariki yanahusisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga, yakionyesha teknolojia mpya za kilimo, ufugaji na uvuvi, huku mamia ya wananchi wakihudhuria kila siku na yamefungwa leo.
MWISHO
Daktari wa mifugo halamshauri ya wilaya ya Maswa,Charles Musira (wa pili kushoto) akitoa maelezo juu ya uboreshaji wa mifugo kwa Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (wa pili kulia) kwenye viwanja vya Maonesho vya Nyakabindi mjini Bariadi.
Wananchi wakiangalia ng'ombe dume aina ya Boran katika banda la maonesho ya mifugo la halmashauri ya wilaya ya Maswa katika viwanja vya Nyakabindi mjini Bariadi.
إرسال تعليق