Na Samwel Mwanga, Maswa.
MBUNGE anayemaliza muda wake wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Mashauri Ndaki, ameibuka mshindi katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kupata kura 5,212, akiashiria nafasi nzuri ya kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu ujao.
Ndaki ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo, amewashinda kwa tofauti kubwa wagombea wengine watano waliokuwa wakichuana naye kuwania ridhaa ya wanachama wa CCM.
Miongoni mwa waliowania nafasi hiyo ni Dkt. Zeye Masunga aliyepata kura 1,055, akifuatiwa na Joseph Bukoye aliyepata kura 550, Magreth Kuhanwa kura 304, Aron Mboje kura 191 na Jonathan Masalamado aliyepata kura 139.
Kura hizo za maoni ni sehemu ya mchakato wa ndani ya chama hicho tawala unaolenga kuwachuja wagombea kabla ya kuwapitisha rasmi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Kwa ushindi huo, Ndaki anasubiri uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM iwapo atateuliwa rasmi kupeperusha bendera ya chama hicho kwa awamu nyingine katika jimbo hilo.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق