Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha (kushoto) akimkabidhi mwenge wa uhuru, Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano (kulia) katika kijiji cha Njiapanda wilayani humo.Na Samwel Mwanga, Maswa
KWA kishindo cha hamasa na uzalendo, Mwenge wa Uhuru umekimbizwa umbali wa kilomita 82 katika Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, na kuzindua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 2.74, inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
Vijana, wanawake, wazee na watoto walijitokeza barabarani kushuhudia tukio hilo leo Agosti 9,2025 huku wakipunga bendera ya taifa na kuimba nyimbo za mshikamano, huku Mwenge ukipita katika mitaa na vijiji ukiacha alama ya matumaini na mshikamo wa kitaifa.
Miongoni mwa miradi mikubwa iliyoguswa ni ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa na ujenzi wa Daraja la Malita, miradi ambayo inalenga kuboresha huduma za afya na miundombinu ya usafiri.
Mbali na miradi ya huduma za jamii, Mwenge umezindua miradi miwili ya kiuchumi ambayo ni biashara ya mkaa mbadala wa Kikundi cha Wanawake na Samia, pamoja na mradi wa uchoraji na uchapishaji fulana na mabango wa kikundi cha vijana cha Maswa Sign.
Pia umeweka mawe ya msingi na kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na matundu ya choo katika Shule ya Msingi Funika. Miradi mingine ni nyumba ya mkuu wa idara na ujenzi wa mradi wa maji katika Vijiji vya Buyubi, Dodoma na Ikungulyasubi.
Akizungumza katika kijiji cha Funika wilayani humo,Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano Anney, amesema kati ya Sh bilioni 2.74 zilizogharimu miradi hiyo, Serikali Kuu imetoa Sh bilioni 2.63, wananchi Sh milioni 4.22 na Halmashauri ya Wilaya Sh milioni 113.63.
“Miradi hii imegusa maisha ya wananchi wa Maswa. Naahidi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa itatunzwa na kuendelezwa ili iendelee kutoa huduma muda wote,” amesema.
Pongezi kwa Usimamizi Bora
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi, aliipongeza wilaya ya Maswa kwa usimamizi mzuri wa miradi na mshikamano wa wananchi.
“Nawapongeza viongozi wa wilaya, hususan Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa kwa usimamizi bora na kuunganisha wananchi katika shughuli za maendeleo,” amesema.
Sauti za Wananchi.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria katika mbio hizo za mwenge katika miradi tofauti tofauti wameeleza furaha na matumaini yao kutokana na miradi hiyo.
“Nimefurahi kuona daraja la Malita likijengwa. Sasa tutasafiri bila hofu ya kukwama wakati wa mvua,” amesema Janeth Paul, mkazi wa Kijiji cha Malita.
Naye Paul Masanja mkazi wa kijiji cha Buyubi amesema kuwa kwa sasa watapunguza muda wa kutafuta maji kutokana na mradi wa maji kukamilika.
“Mradi wa maji Buyubi ni faraja kwetu, tutapunguza muda wa kutafuta maji na kuutumia kwenye shughuli za kiuchumi,” amesema.
Masumbuko John ni kijana wa mjini Maswa amesema kuwa kwa sasa vijana wasisubiri kuajiriwa ni vizuri wakawa wabunifu kwa kujiajiri kama walivyofanya vijana wa kikundi cha Maswa Sign.
“Hii miradi ya vijana kama Maswa Sign inatupa mfano kwamba vijana tukijipanga tunaweza kujiajiri na kusaidia familia,” amesema.
Awali Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anamringi Macha aliupokea mwenge wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mboni Mhita na baadaye naye alimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dkt Vicent Naano Anney ili kuukimbiza katika wilaya hiyo.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya Mwenge wa Uhuru ni “Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani,”
Mwisho.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa mwaka 2025,Ismail Ussi (aliyekati) akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya msingi Funika wilaya ya Maswa.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, Ismail Ussi akizungumza na wananchi wa kijiji cha Funika wilaya ya Maswa.
Sehemu ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa wakiwa katika uzinduzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Msingi Funika yaliyozinduliwa na Mwenge wa uhuru mwaka 2025.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akiwa ameshika Mwenge wa uhuru 2025.

إرسال تعليق