Bwawa la New Sola lajaa maji.


Sehemu ya Bwawa la New Sola katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu likiwa limejaa kufuatia watu kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi ya bwawa hilo


Mkurugenzi Mtendaji WA Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias akielezea jinsi Maji yalivyojaa kwenye bwawa la New Sola lililoko katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kufuatia kutunza Kwa vyanzo vya hifadhi ya moto inayoingiza Maji kwenye bwawa hilo.

 

Na Samwel Mwanga,Maswa.

 

BWAWA la Maji la New Sola (maarufu bwawa la Zanzui )lililo katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu limejaa maji ambayo yamezidi uwezo wa bwawa hilo na  sasa maji yaliyozidi  yanapita kwenye utoro wa maji wa bwawa hilo kuelekea mto Simiyu.

 

Bwawa hilo ndicho chanzo kikuu cha  maji kwa wakazi wapatao 120,000 wa mji wa Maswa na vijiji 12 vinavyotumia maji hayo.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa) Mhandisi Nandi Mathias amesema kuwa bwawa hilo limejaa maji kutokana na Mkuu wa wilaya hiyo,Aswege Kaminyoge na Kamati mzima ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo kuwataka kuhifadhi vyanzo vya Maji vinavyoingiza Maji kwenye bwawa hilo.

 

Amesema kuwa walielekeza nguvu kubwa kulinda hifadhi hasa mto Sola kwa kuzuia wananchi waliojitokeza  kufanya shughuli za kilimo kwenye hifadhi hiyo mwezi Disemba mwaka jana.

 

Mhandisi Nandi amesema kuwa kutoka na jitihada hizo za kulinda chanzo cha mto huo ambao unachangia asilimia  75 ya maji yote yanayoingia katika bwawa hilo matokeo yake kwa mvua zilizonyesha Mwezi Disemba mwaka jana hadi kufikia Januari 18 mwaka huu,bwawa la New Sola lenye uwezo wa kujaa lita Bilioni 5 za maji limejaa zaidi ya hapo.

 

"Mto Sola ndiyo unaingiza Maji asilimia 75 kwenye bwawa letu la New Sola ndiyo maana Mkuu wa wilaya na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ilitutaka kuwekwa nguvu kubwa Kwa kusaidiana nao kuhakikisha chanzo hicho kinalindwa Kwa gharama zozote,"amesema.

 

Amesema kwa sasa bwawa limefikia kikomo chake na maji yaliyozidi yanaondoka kupitia utoro wa maji wa bwawa hilo na kuelekea mto Simiyu unaopeleka Maji yake katika Ziwa Victoria Ili kuweza kunusuru uhai wa Bwawa la New Sola.

 

 Mhandisi Nandi ametoa wito kwa Wananchi wa vijiji vinavyolizunguka bwawa hilo kuendelea kutunza Mazingira ya hifadhi ya bwawa hilo sambamba na mito inayotiririsha  maji kuelekea kwenye bwawa la New Sola ukiwemo mto Mwakungwe na mto Gasela.

 

Aidha ameishukuru serikali ya awamu ya sita baada ya kulipa fidia kwa wananchi wa  Kijiji cha Zanzui waliokuwa na maeneo ya kulima katika hifadhi ya  bwawa hilo na kupisha chanzo cha maji kwa sasa bwawa lina uhakika wa kuhifadhi maji takribani meta za ujazo  million  5 .

 

Mhandisi Nandi pia ameishukuru serikali ya wilaya ya Maswa inayoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo,Aswege  Kaminyoge kwa kuendeleza usimamizi madhubuti wa vyanzo vya maji ukiwemo mto Sola.

 

Pamoja na jitihada hizo zinazofanywa na Serikali ya wilaya na Mauwasa kulinda hifadhi ya bwawa hilo bado wapo baadhi ya wafugaji wachache wamekuwa wakiingiza mifugo yao bwawani.

 

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge amesema kuwa vyanzo vya Maji vikitunzwa na kuhifadhiwa vizuri vitasaidia vizazi vijavyo na hivyo kuwataka Viongozi wa vijiji vinavyolizunguka bwawa hilo kuhakikisha hakuna wafugaji wanaopeleka mifugo kwenye bwawa hilo.

 

"Faida ya kutunza na kuhifadhi vyanzo vya Maji ndiyo hii tumeiona maana bwawa limejaa Maji kabla hata ya mvua za masika hivyo tuendeleze utamaduni huu wa kutunza Mazingira na wale wachache wanaoingiza mifugo ndani ya bwawa naagiza viongozi wa maeneo hayo kuhakikisha jambo hilo linaachwa mara mara moja,"amesema.

 

MWISHO.

 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم