Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki,Stanslaus Nyongo(mwenye shati jeupe)akitembelea soko Kuu la mji wa Maswa mkoa wa Simiyu kujionea hali halisi ya uchakavu WA soko hilo ambalo limeanza kukarabatiwa. |
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki,Stanslaus Nyongo akihutubia kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Stendi ya Zamani mjini Maswa mkoani Simiyu. |
Na Samwel Mwanga,Maswa.
SOKO Kuu la mji wa Maswa katika mkoa
wa Simiyu limeanza kufanyiwa ukarabati ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mbunge
wa Jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo (CCM) aliyoitoa wakati wa kampeini
za uchaguzi Mkuu uliopita.
Jumla ya Sh Milioni 114.5
zinatarajia kutumika kukarabati soko hilo ambalo limejengwa zaidi ya miaka 80
iliyopita katika wilaya ya Maswa na hivyo kuanza kuchakaa.
Nyongo akihutubia mamia ya wakazi wa
Mji huo katika viwanja vya Stendi ya zamani amesema kuwa katika kiasi
hicho cha fedha za ukarabati huo ametoa Sh Milioni 97.5 kupitia mfuko wa Jimbo
la Maswa Mashariki.
Amesema kuwa awamu ya kwanza kupitia
mfuko huo ametoa Sh 42,596,000/- na sasa ametoa kiasi cha Sh 55,000,000/-na
Hamashauri ya wilaya hiyo ikitoa kiasi cha Sh 17,000,000/- ili kuunga mkono
jitihada zake za kuhakikisha kuwa mji huo unakuwa na soko la kisasa.
"Kupitia mfuko wa jimbo la
Maswa Mashariki katika awamu ya kwanza tumetoa Sh Milioni42.5 na sasa
tumeidhinisha Sh Milioni 55 na Halmashauri ya wilaya ya Maswa imeniunga mkono
kwa kutoa kiasi cha Sh Milioni 17,"
"Kwa kiasi hiki cha fedha
tunakwenda kuwa na soko la kisasa lenye kufanana na Mji wetu ambao kwa sasa
umebadilika sana hivyo niwashukuru madiwani kwa kuweza kuidhinisha kiasi cha
fedha kutoka halmashauri ili kuniunga mkono katika ukarabati huu,"amesema.
Aidha amewataka wasimamizi wa
ukarabati huo kuhakikisha kazi hiyo inamalizika kwa wakati ili wafanyabiashara
wafanye shughuli zao katika mazingira mazuri ya kuwahudumia wananchi wanaotumia
soko hilo kujipatia mahitaji yao ya kila siku.
Awali Afisa Mtendaji wa Kata ya
Sola,Roselyne Kinawiro akisoma taarifa ya utekelezaji wa ukarabati huo mbele ya
Mbunge Nyongo amesema kuwa hadi sasa kiasi cha Sh 39,331,683/-ndizo zimetumika.
Amesema kuwa hadi sasa kazi
mbalimbali zimefanyika zikiwemo za kusafisha eneo la Ujenzi,kuchimba
msingi,kuchimba mashimo ya mabomba na kumwaga jamvi la chini.
Kazi nyingine zilizofanyika ni
pamoja na kujenga ukuta,kusimika mabomba na kumwaga Bim ya msingi na kazi hizo
zote zimefanyika kwa kiwango kikubwa kulingana na mkataba waliofunga na
fundi,Issa Buchwa.
Naye Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege
Kaminyoge pamoja na kumpongeza mbunge huyo kwa kusimamia maendeleo katika Jimbo
lake amemhakikishia naye kusimamia fedha zote za miradi zinazoletwa na serikali
kwenye wilaya hiyo.
MWISHO.
إرسال تعليق