Na Mwandishi wetu, Simiyu.
Katika kuhakikisha agizo la Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philipo Mpango kwa wakuu wa
Mikoa kuhakikisha wanapanda miti kwenye maeneo yao, Mkoa wa Simiyu umezindua
rasmi zoezi hilo.
Katika uzinduzi wa zoezi hilo ambalo
limefanyika Mjini Bariadi na kuwashirikisha wananchi, viongozi wa serikali na
siasa, wanafunzi na wanamichezo.
Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Yahya Nawanda
ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema kuwa mkoa wa Simiyu imejipanga kupanda miti
Milioni 9.
Kiongozi huyo amesema kuwa kila
Wilaya imepewa malengo kwenye maeneo yake, ambapo amewaagiza wakuu wa Wilaya
mkoani humo kuhakikisha agizo la Makamu wa Rais linatekelezwa kwa kasi kubwa.
Amesema kuwa mbali na miti hiyo
kupandwa, lakini ilindwe ili isiweze kuharibika ikiwa pamoja na kuzuia wananchi
kuharibu kwa kuchungia mifugo yao, ambapo amewataka wananchi kuacha tabia ya
kukata miti.
“ Agizo la Makamu wa Rais lazima
litekelezwe na wakuu wa Wilaya wote hakikisheni mnakwenda kupanda miti, Mkoa
tumejipangia kupanda miti Milioni 9 mwaka huu, na hili linawezekana kila mmoja
ahakikishe anatekeleza” amesema Dkt. Nawanda.
Amewataka wananchi kujenga tabia ya
kupanda miti kwenye maeneo yao huku akikisitiza kuacha tabia ya kukata ovyo miti,
ambapo kwenye uzinduzi wa zoezi hilo, mkuu huyo wa mkoa amegawa bure miche ya
matunda kwa wananchi waliohudhuria.
Awali akizungumza kwenye zoezi hilo,
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange, amesema kuwa kama Wilaya
wamejipanga kuhakikisha wanapanda miti kwenye taasisi zote za serikali na
binafsi.
Kapange amesema kuwa kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali, kikiwemo kiwanda cha kuchambua pamba Alliance
Ginnery, tayari wameanza kupeleka miche ya miti kwenye taasisi mbalimbali
zikiwemo shule na vituo vya kutolea huduma za Afya.
Naye Ofisa Maliasili na Mazingira
Halmashauri ya Mji wa Bariadi Monica Deusdedit amewataka wananchi kufuata
taratibu zote zinazotakiwa katika kukata miti.
إرسال تعليق