Bweni la wanafunzi kike katika shule ya Sekondari Bukundi Wilayani Meatu Mkoani Simiyu. |
Na Bahati Sonda, Meatu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu dkt Yahya Nawanda ameagiza
wanafunzi 103 wa kike wanaosoma katika Shule ya Sekondari Bukundi iliyopo
katika wilaya ya Meatu mkoani humo wakae bweni mara baada ya ujenzi wa mradi wa
bweni shuleni hapo utakapokamilika.
Amesema kuwa wanafunzi hao wanatakiwa kukaa bweni
mara tu baada ya ujenzi huo kukamilika ili wapate muda wa kutosha kujisomea
hususani nyakati za usiku hali itakayosaidia kuinua viwango vyao vya ufaulu.
Dkt Nawanda ametoa agizo hilo mapema leo kwa
uongozi wa Wilaya hiyo wakati akikagua utekelezaji wa bweni la wanafunzi katika
Shule hiyo na kusema hatua hiyo itawapunguzia changamoto mbalimbali ikiwemo
kuondoa utoro pamoja na mimba za utotoni zinazosababishwa na vishawishi
mbalimbali wanavyokutana navyo njiani wakati wakiwa wanaenda shule.
Aidha ametoa masaa 48 kwa Mkuu wa Wilaya hiyo
kamati ya ulinzi na usalama wa Wilaya kuhakikisha wanafunzi 28 wa kidato cha
kwanza shuleni hapo ambao hawajaripoti wawe wameripoti.
Nyabuho Ndege na Amina Ally ni wanafunzi wa shule
hiyo wamebainisha kuwa uwepo wa bweni hilo utawasaidia kukabiliana na tatizo la kutembea umbali mrefu kwani wengi
wao wanatembea umbali wa kilometa 5 hadi 8 kutoka nyumbani hadi kufika shuleni
kila siku.
Aidha wameeleza kuwa kutokana na umbali huo iliyokuwa
ikipelekea kukosa vipindi vya Asubuhi kwani walikuwa wanatoka nyumbani saa 12 Asubuhi
na kufika shuleni saa 4 wakati huo wakifika shule wakiwa wamechoka hivyo
kushindwa kusoma vizuri kwa sababu ya uchovu.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni hilo
Katibu wa Kamati ya usimamizi wa mradi Barnabas Sombi amesema kuwa mradi umegharimu
kiasi cha Milioni 130.8 ambao umefikia asilimia 98 na unatekelezwa kupitia pesa
za Tasaf na hatua ya utekelezaji iliyobaki ni utengenezaji wa vitanda 40 na
milango 15 ambapo tayari mafundi wamepatikana na wapo katika hatua za mwisho za
ukamilishaji.
Sombi ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa
kupunguza hatari ya mimba za utotoni kwa wanafunzi wanaoishi katika nyumba za
kupanga mitaani pasipo uangalizi wa wazazi au walezi, kuweka mazingira mazuri
ya kufundisha na kujifunza kwa vitendo hasa kwa masomo ya sayansi ili kuongeza
ufaulu wa wanafunzi.
Mwisho.
إرسال تعليق