Takukuru maswa yaja na program ya ‘Takukuru-Rafiki’

 


Kaimu Mkuu wa Takukuru wilaya ya Maswa,Alpha Malisa akitambulisha program ya Takukuru-Rafiki kwa wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Wilaya hiyo(hawapo pichani)katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo


 

Na Samwel Mwanga,Maswa.

 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) katika Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imetambulisha Program mpya iitwayo TAKUKURU-Rafiki ili kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau katika kukabili tatizo la rushwa katika utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 

Kaimu Mkuu wa Takukuru wilaya ya Maswa,Alpha Malisa akitambulisha program hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo amesema kuwa itatekelezwa katika ngazi ya Kata kwa ajili ya kutambua kero zilizopo kwenye utoaji na upokeaji wa huduma za kijamii kama vile Elimu au Afya pamoja na mchakato wa kutekeleza miradi ya maendeleo kama Ujenzi wa miundombiniu ya Maji.

 

Amesema kuwa Kwa kufanya hivyo watatambua kero ambazo zikiachwa pasipo kutatuliwa au kupatiwa ufumbuzi zinaweza kusababisha kutokea Kwa vitendo vya Rushwa.

 

"Hii program itaanzia kwenye ngazi ya Kata na diwani wa Kata ndiye atakuwa Mwenyekiti wa vikao hivyo na huko tutatambua kero zilizoo kwenye jami hasa katika kutekeleza hii miradi ya maendeleo inayopeleka na serikali huko Kwa Wananchi,"

 

"Pia program hii inaakisi maana ya neno rafiki kwa kubeba dhana ya kuwa karibu na kushirikiana na Wananchi na wadau kuondoa kero katika jamii,"amesema.

 

Amesema kuwa moja ya faida ya program hiyo itachangia kukuza Ustawi wa utawala bora kwa kuzuia vitendo vya rushwa visitokee katika utoaji wa huduma kwa Umma au katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 

"Hii itachangia kuboresha huduma zinazolewa na Umma na wadau wengine pia kuokoa fedha kwa kujengwa na kutekelwzwa miradi bora,endelevu na inayokidhi thamani ya fedha iliyotumika.

 

Aidha Malisa ametoa wito kwa Wananchi kushirikiana na Takukuru kuzuia vitendo vya rushwa visitokee katika njia ya utoaji wa huduma kwa Umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo wananchi wasikae penbeni katika kutekeleza program hiyo Ili kwa pamoja kuijenga Tanzania.

 

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge amesema kuwa iwapo program hiyo ikitekelezwa itapunguza au kuondoa vitendo vya rushwa katika jamii hivyo ameiomba jamii kuipokea na kulifanyia kazi.

 

"Hii program ikitekelezwa kama tulivyoelezwa na Kaimu Mkuu wa Takukuru wilaya ya Maswa nina imani itapunguza au kuondoa vitendo vya rushwa katika jamii hasa katika miradi ya maendeleo inayopelekwa na serikali kwa Wananchi.

 

Mwisho

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post