Madiwani Maswa wakiwa katika Kikao Cha Baraza la Madiwani |
Na Samwel Mwanga,Maswa.
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu limepitisha makadirio ya bajeti ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa)wilayani humo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mkutano huo maalum wa baraza hilo umefanyika katika ukumbi wa" mikutano wa Halmashauri ya Wilaya hiyo na kupitisha makadirio ya bajeti yenye jumla ya Shilingi Bilioni 6.0
Akiwasilisha bajeti hiyo katika mkutano huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Maswa,Mhandisi Lucas Madaha alisema kuwa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 5.00 zitatumika katika maendeleo ya miradi ya Maji wilayani humo.
Mhandisi Madaha alisema kuwa fedha nyingi wamezielekeza kwenye miradi ya maji Ili kuweza kuongezeka hali ya upatikaji wa maji vijijini katika wilaya hiyo ambao Kwa Sasa uko kwa kiwango cha asilimia 74.69.
"Ukiangalia kwenye bajeti yetu hii kiasi cha fedha ambazo ni nyingi shilingi bilioni 5 zimeelekezwa kwenye miradi ya maji,"
"Kwa sasa hali ya upatikanaji wa Maji vijijini kwenye wilaya yetu ni asilimia 74.69 hivyo tunataka tufikie malengo yetu ya asilimia 85 hadi kufikia mwaka 2025 kama inayotutaka Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),"alisema.
Mhandisi Madaha ameitaka miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ukamilishaji wa Mradi wa Maji WA Kijiji Cha Zabazaba,Kujenga miradi ya maji ya vijiji vya Budekwa, Ipililo,Funika na Ngongwa-Kulimi
Miradi ya maji itakayopanuliwa ni Ile ya vijiji vya Inenwa-Kizungu,Malekano-Kadoto, Nguliguli-Mwamanenge,Jija-Igunya ,Njiapanda-Nhelela na Masamwa -Ishima.
Ameendelea kueleza miradi mingine ni pamoja na kufanya utafiti Ili kuchimba visima saba vijijini,Kuboresha visima 10 vya mikono na kuwekwa mfumo WA pampu za kutumia umeme wa jua(Solar) na kuwekwa tenki la ujazo wa Lita 5000 na kuongeza vituo vinne kila kisima kurahisisha uchotaji wa Maji.
Mhandisi Madaha amevitaja vyanzo vya mapato ya fedha Ili kukamilisha bajeti hiyo ni pamoja na Ripa kwa matokeo (P for R) Sh 5,164,208,400 Mfuko wa Maji wa Taifa Sh 872,774,679.18 na Matumizi ya kawaida (OC) Sh 25,395,000.
Akizungumza changamoto walizonazo alisema ni pamoja na uhaba wa vitendea kazi yakiwemo magari,upungufu wa Watumishi,kuchelewa kutolewa Kwa fedha na Uhaba wa vyanzo vya Maji vya Uhakika.
Baadhi ya madiwani wakichangia bajeti hiyo walisema kuwa licha ya Ruwasa kufanya kazi nzuri na kubwa ya kuhakikisha upatikanaji wa Maji safi na salama kwenye maeneo ya vijijini ni vizuri Sasa wakaongeza nguvu.
Wamesema kupatikana Kwa Maji safi na salama hasa maeneo ya vijijini kutaondoa magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa hatari wa kipindipindu.
"Maji safi na salama yakipatikana Kwa umbali mfupi kutoka makazi ya wananchi wetu kuna faida nyingi na baadhi yake ni pamoja na kuondoa magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa kipindipindu,"alisema Esther Ngolongho diwani wa Kata ya Budekwa.
Mwisho.
Post a Comment