Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu Mohamed akizungumza na mamia wa wanachama wa Chama hicho Wilaya ya Itilima kwenye sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM. |
Na
Derick Milton, Itilima.
Chama cha mapinduzi (CCM) kimetoa utaratibu mpya
wa utolewaji wa kadi za uanachama kwa mwanachama mpya, kuwa lazima awe umesoma
Darasa la Itikadi kwa muda wa miezi mitatu.
Akitangaza utaratibu huo mpya leo mbele ya mamia
wa wanachama wa Chama hicho Wilaya ya Itilima kwenye sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa
kwa chama hicho katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu Mohamed Ali amesema kuwa utaratibu
wa zamani hautakuwepo tena.
Amesema madarasa hayo yatakuwepo kwenye kila kata,
ambapo vijana wote watatakiwa kushiriki mafunzo hayo ambayo yatakuwa yanatolewa
kwenye kata husika na mara baada ya kuhitimu kwa kipindi cha miezi mitatu ndipo
watapewa kadi.
Amewaagiza watendaji wa Chama hicho ngazi za
Wilaya hadi kata, kuhakikisha wanakwenda kuanzisha madarasa hayo kwa mujibu wa
maelekezo yaliyotolewa na chama hicho na masomo yaanze mara moja.
“ Sasa chama kimekuja na utaratibu mpya wa kutoa
kadi za uanachama kwa wanachama wapya, ili uweze kupata kadi lazima upitie
kwenye mafunzo ya Itikadi kwa muda wa miezi mitatu ndipo utapata kadi, bila ya
hivyo hautapata kadi, ule utaratibu wa zamani hautakuwepo tena” amesema Ali….
“ Niwaagize watendaji wa CCM Wilaya ya Itilima,
mkimaliza sherehe hizi, nendeni mkaazishe madarasa hayo kwenye kila kata, kwa
kufuata taratibu ambazo zimetolewa,” ameongeza Ali.
Amesema Chama hicho kimekuja na utaratibu huo
mpya, ili kadi zinazotolewa kwa wanachama wapya, lazima ziwe na adhi kama chama
kilivyo.
MWISHO.
Post a Comment