Mbunge wa Jimbo la Itilima Mkoani Simiyu Njalu Silanga akizungumza na wananchi wa Jimbo lake la Itilima, wakati wa sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika kiwilaya katika kijiji cha Ndoleleji. |
Na
Derick Milton, Itilima.
“ Nilianza harakati za siasa mwaka 2007 baada ya
vijana wa Mkoa wa Simiyu kuniamini kwa kunipigia kura 664, kati ya kura 668,
vijana wanne tu ndiyo walisema sitoshi kuwa mjumbe wa Mkutano mkuu CCM”
Ni maneno yake Mbunge wa Jimbo la Itilima Mkoani
Simiyu, Njalu Daudi Silanga (CCM), anatajwa kuwa mbunge namba moja ndani ya
mkoa huo anayeungwa mkono zaidi na wananchi wote wa jimbo lake hata wale kutoka
vyama shindani.
Hadi anafikia hatua ya kuwa mwakilishi wa wananchi
wa jimbo hilo kwenye chombo cha kutunga sheria (bunge), Njalu anasema haikuwa
kazi rahisi kupambana na vigogo wa siasa kutoka vyama shindani.
Kutoka mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Mjumbe wa
Halmashauri kuu ya CCM (MNEC) na Mbunge wa Jimbo la Itilima, alisukumwa zaidi
na mateso ya wananchi wa jimbo hilo waliyoyapata kwa miaka 20.
Chini ya vigogo wa siasa John Cheyo (UDP), Dany
Makanga (UDP) na wengine wengi wakiwemo Edward Ng’wani, zaidi ya miaka 20
wananchi waliteseka na miundombinu mibovu ya Barabara.
Ukosefu wa huduma za Afya ilikuwa changamoto
nyingine iliyowatesa, ukosefu wa maji safi na salama, kutokuwepo kwa mazingira
rafiki ya upatikanaji wa elimu iliyo bora kwa wananchi wa Jimbo hilo.
Utekelezaji
wa Ilani.
Wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
Ilani ya CCM kwa wananchi wa Jimbo hilo jana, wakati wa sherehe za miaka 46 ya
kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika katika kijiji cha Nangale kata ya Ndoleleji.
Anasema baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka
2015, kazi yake ya kwanza ilikuwa kuhakikisha anatatua changamoto ya
miundombinu ya Barabara ambayo ndiyo ilikuwa kilio kikubwa cha wananchi.
“ Nikiwa na Madiwani 7 kutoka CCM kati ya 22,
tulifanya kazi kubwa usiku na mchana ya kuhakikisha jimbo la Itilima linabadilika,
wananchi wanaanza kuonja raha ya maendeleo na kupata huduma bora za kijamii,”
anasema Njalu.
Miundombinu
ya Barabara.
Mbunge huyo anasema kuwa kwa kipindi cha miaka
saba, Wilaya ya Itilima imefunguka, kila sehemu panapitika kwa nyakati zote
tofauti na ilivyokuwa awali ambapo hakuna gari ilifika kijijini.
Anaeleza kuwa Wilaya hiyo inazo Barabara kubwa na
muhimu zipatazo 82, ambapo kwa sasa Barabara zote zimefunguliwa na zinapitika
muda wote na wananchi wanafanya shughuli zao kwa furaha.
“ Kila mwaka nimekuwa nikihakikisha tunatapa fedha
za kutengeneza Barabara zetu, kwa sasa unaweza kuingia na kutoka Wilaya ya
Itilima kwa kupitia sehemu yeyote, hakuna kikwazo hata kimoja”…..
“ Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suruhu Hassan
kwa kuendelea kutuletea fedha nyingi kwenye eneo la Barabara, na katika bajeti
ya mwaka huu ametupatia kiasi cha Sh. Bilioni 2.7 kwa ajili ya Barabara tu,”
anasema Njalu.
Huduma
za Afya.
Njalu anasema kuwa wakati anaomba kura kwa wananchi
kipaumbele chake cha pili ambacho aliwahidi wananchi, ni kuhakikisha wanapata
huduma bora za Afya na kwa karibu.
Anasema jambo la kwanza kulifanyia kazi baada ya
kuchaguliwa, lilikuwa kuhakikisha Wilaya hiyo inapata Hospitali ya Wilaya,
jambo ambalo alilifanikisha kwa kiwango kikubwa na Wilaya ina Hospitali ya
Wilaya.
“ Wananchi sasa hawafuati huduma Wilayani Bariadi,
Hospitali yetu inafanya kazi na inatoa huduma zote, Rais Dkt. Samia ametulileta
Milioni 500 kwa ajili ya kuboresha Hospitali yetu na tunaendelea na maboresho”
Anasema kuwa kwa kipindi cha Mwaka mmoja wa Rais
Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati 8 pamoja na ujenzi wa
kituo kingine kimoja cha Afya cha Mwanunda na kimekamilika.
Elimu.
Anasema kuwa Wilaya hiyo ilikuwa nyuma kielimu
kutokana na mazingira, huku mwitikio wa wananchi kupeleka watoto shule ukiwa
chini, ambapo kwa kushirikiana na wananchi wameweza kujenga shule mpya 16.
“ Katika Elimu tunaishukuru serikali imeendelea
kuboresha mazingira, tumepokea zaidi ya Bilioni 3 kwa ajili ya kuboresha
mazingira ya wanafunzi na walimu kwa kujenga madarasa na nyumba za walimu,”
anaeleza Silanga.
Huduma
ya maji.
Chagamoto kubwa nyingine ambayo wananchi wa jimbo
hilo wameteseka nayo kwa muda mrefu ni upatikanaji wa maji safi na salama,
ambapo awali walipata maji kwenye madimbwi na mabwawa ya kuchimba wenyewe.
Mbunge huyo akizungumzia suala la huduma ya maji,
anaeleza kuwa kwa kiwango kikubwa huduma hiyo imeboreshwa, na wananchi maeneo
mengi wameanza kuonja maji safi na salama.
“ Pale makao makuu yetu ya Wilaya Lagangabilili,
walikuwa hawajawahi kupata maji safi na salama, lakini nilipoingia nilihakikisha
tunapata mradi mkubwa wa maji, na sasa wanapata maji kila siku … maji safi na
salama”
“ Katika kijiji hiki cha Ndoleleji serikali
imeleta kiasi cha zaidi ya Sh. Milioni 192 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu
cha maji, muda siyo mrefu tutapata maji safi na salama hapa”
Anaeeleza kuwa mbali na hilo, kuna mradi mkubwa wa
kutoa maji ziwa Victoria, ambapo Jimbo lake limewekwa katika awamu ya kwanza ya
mradi huo, hivyo wananchi watarajie kupata maji kutoka ziwa Victoria.
Huduma
ya Umeme.
Njalu anasema kuwa hadi kufikia Mwezi Aprili mwaka
huu, vijiji vyote 102 katika jimbo hilo vitakuwa na umeme, ambapo baada ya hapo
wataanza kupeleka umeme kwenye vitongoji.
“ Serikali ya Mama Samia, tayari imetutengea kiasi
cha Sh. Bilioni 14 kwa ajili ya kusambaza umeme, ambapo Mkandarasi Sengerema
Company Ltd anaendelea na zoezi la kupeleka umeme katika vijiji vyote” anasema
Njalu.
Michezo.
Mbunge huyo anasema kuwa suala la michezo halijaachwa
nyuma, kwani tangu amechaguliwa alianzisha mashindano ya Njalu Cup, mashindano
ya mpira wa miguu ambayo yamekuwa maarufu na kuleta furaha, amani na upendo
baina ya wananchi wa jimbo hilo.
Hata hivyo Mbunge huyo anasema kuwa kazi bado
haijamalizika katika jimbo hilo, kwani baadhi ya maeneo bado yameendelea kuwa
na changamoto, ambapo yeye na viongozi wa Wilaya wakiwemo madiwani wataendelea
kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa.
Anasema kuwa kuendelea kuwa Mbunge kwenye jimbo
hilo, atahakikisha anawatumikia wananchi wa jimbo hilo kwa nguvu zote, ikiwa
pamoja kuhakikisha anashirikiana nao katika kuleta maendeleo.
“ Kazi bado haijaisha, tuliteseka sana miaka 20,
lakini sasa tuna miaka 7 tumeanza kuonja matunda, kazi bado haijamalizika, mimi
pamoja na viongozi wengine na madiwani, tumesema lazima tuwatumikie”
Njalu anawataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa
serikali na wadau wa maendeleo, ikiwemo kupeleka watoto shule kwani kazi kubwa
imefanyika ya kuboresha elimu mashuleni.
“ Kwenye Wilaya hii, chini yangu, chini yangu, na
kwa umri wangu huu, hakuna mwananchi atateseka kama ambavyo mliteseka miaka 20
nyuma, tumejipanga kuhakikisha tunawahudumia,” amesema Njalu.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment