MJUMBE wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC) Gungu Silanga akihutubia Wana chama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 46 ya Kuzaliwa kwa CCM, yaliyofanyika kimkoa katikwa viwanja vya Madeco mjini Maswa.
Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu kimeitaka serikali kurejesha usafiri wa magari madogo maarufu kama Michomoko iliyokuwa imezuiliwa kutokana na ajali zilizokuwa zimekithiri.
Itakumbukwa kuwa Julai 13, 2022, Serikali mkoani Simiyu ilipiga marufuku usafiri wa magari madogo baada ya kutokea ajali iliyosababisha vifo vya watu watano na kujeruhi wengine 11 eneo la Magereza nje kidogo ya Mji wa Bariadi.
Akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika katika viwanja vya Madeco mjini Maswa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa Gungu Silanga ameiomba serikali kurejesha usafiri huo uliokuwa umeajiri vijana wengi.
Amesema vijana wengi katika Mkoa wa Simiyu walikuwa wamejiajiri kupitia usafiri na usafirishaji wa abiria na bidhaa mbalimbali na kwamba kuzuiliwa kwa magari hayo kumesababisha vijana kukosa ajira.
‘’Vijana walikuwa wamejiajiri kupitia magari madogo, tuangalie namna nzuri ya kurejesha usafiri huo…ni mkoa pekee uliokuwa umezuia michomoko, serikali iwasaidie ili vijana wafanye kazi’’ amesema Gungu.
Amesema kupitia magari hayo vijana wengi walikuwa wanajipatia fedha, lakini hadi sasa vijana hao wamepoteza ajira hali iliyowakatisha tamaa pia imepunguza mapato ya serikali katika mkoa wa Simiyu.
Amelitaka Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na serikali kukaa na vijana hao ili kubaini changamoto na kuwapa maelekezo ili atakayevunja sheria aweze kuchukuliwa hatua yeye mwenyewe kuliko kuzuia magari yote.
‘’Huwezi kuzuia magari yote wakati aliyesababisha ajali ni mmoja, hivyo viongozi wa serikali na Jeshi la Polisi kaeni na vijana wa michomoko ili kurejesha usafiri huo ili shughuli ziendelee’’ amesisitiza Gungu.
MWISHO.
إرسال تعليق