Raia 74 wa Ethiopia walioko Gereza la Malya wanateseka, wasaidiwe-Hakimu


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa,Enos Missana akizungumza kwenye maazimisho Wiki ya Sheria mwaka 2023.

 

Na Samwel Mwanga,Maswa.

 

HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,Enos Missana ametoa wito kwa jamii kuwasaidia misaada mbalimbali  Wazuiliwa 74 ambao ni  raia wa Ethiopia walioko katika Gereza la Malya lililoko wilayani humo.

 

Akizungumza katika kilele cha Wiki ya Sheria kilichofanyika kwenye Viwanja vya Mahakama ya Wilaya, amesema kuwa Wazuiliwa hao ambao si Mahabusu wala Wafungwa wapo katika Gereza hilo kwa kipindi cha miaka Minne tangu kumaliza adhabu yao.

 

Hakimu Misana ameeleza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo kuwa Wazuiliwa hao wana hali mbaya inayotia huruma kutokana na kutokupata mahitaji yao muhimu kama vile Viatu,Mavazi,Sabuni,Mishwaki na dawa za meno.

 

Amesema kuwa Wazuiliwa hao hawana ndugu ambao wamekuwa wakiwatembelea kama ilivyo kwa mahabusu na Wafungwa wengine walioko kwenye Gereza hilo.

 

"Hawa Wazuiliwa hawana ndugu kama ilivyo kwa mahabusu na Wafungwa walioko kwenye gereza hilo hivyo yale mahitaji ya msingi wanashindwa kuyapata kweli Wana hali ngumu,"

 

"Na kwa sasa wamekuwa wakisaidiwa na Mkuu wa Gereza hilo na wakati mwingine na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo watu hao wanahitaji kusaidiwa,"amesema.

 

Hakimu Missana amezidi kuelezea kuwa wakati wa Wiki ya Sheria mara baada ya kutembea gereza hilo na kutoa Elimu ya sheria pia katika ukaguzi wa Magereza kama yaliyo majukumu yake ya kawaida ndipo alipobaini kuwepo Kwa Wazuiliwa hao ambao kesi zao za Uhamiaji zilishakwisha hivyo wanasubiri Serikali ya nchi yao kuwasafirisha kuwarejesha nchini Ethiopia.

 

Amesema wao wakiwa watumishi wa Mahakama katika wilaya hiyo na Wadau wengine waliweza kuchangishana vitu mbalimbali  kwani kwa mwaka huu wameanzisha kitu kipya  kiitwacho"Tendo la huruma kwa Wenye Uhitaji"  na hivyo kuomba watu wengine walioguswa waweze kuwasaidia kwani hao ni binadamu wenzetu licha ya kutokuwa ni Raia wa nchi yetu.

 

"Kwa taratibu zinavyoonekana hawa Wazuiliwa bado wataendelea kukaa kwenye gereza hilo hivyo niwaombe watu wengine walioguswa waweze kuwasaidia watu hao,"amesema.

 

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge ameuomba Uongozi wa Uhamiaji mkoa wa Simiyu waweze kuharakisha taratibu zinazotakiwa ili raia hao wa Ethiopia waweze kurejeshwa katika nchi yao.

 

Pia amemwagiza Katibu Tawala Wa Wilaya hiyo,Agnes Alex kuandaa utaratibu Ili waweze kufika katika gereza la Malya na kuwaona hao Wazuiliwa.

 

"Niombe Uongozi wa Uhamiaji mkoa wa Simiyu uweze kuharakisha Ili kuhakikisha raia hao wa Ethiopia waliozuiwa katika gereza la Malya wanaweza kurejeshwa kwao pia Katibu Tawala Wa Wilaya andaa utaratibu tukawaone kama walivyofanya watumishi wa Mahakama,"amesema.

 

MWISHO.

 


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post