DC Kaminyoge akagua Miradi ya Maendeleo Maswa.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge (mwenye shati rangi ya kijani) akitoa maelezo kwa mmoja wa mafundi wanaojenga shule mpya ya msingi ya Mwabaraturu.

 

Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,Aswege Kaminyoge (aliyepo mbele mkono wa kulia) akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo na Watumishi WA Halmashauri ya wilaya ya Maswa baada ya kukagua Ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya Msingi Mwawayi.

 

 Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge (aliyeko mbele mwenye kaunda suti rangi ya bluu) akiwa anakagua ukarabati wa madarasa katika shule ya msingi Shanwa.

 

Na Samwel Mwanga, Maswa.

 

MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge amefanya ziara ya siku mbili ya kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo katika sekta za Elimu na Afya.

 

Katika ziara hiyo Kaminyoge, ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo pamoja na  timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya wilaya ya Maswa. 

 

Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa kwenye miradi hiyo amekuwa akisisitiza kufuatwa kwa utaratibu wa manunuzi ya vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na  iweze kutumika.

 

Amesema maendeleo ya ujenzi kwa ujumla ni mazuri ambapo asilimia kubwa ya miradi ipo katika hali nzuri isipokuwa miradi michache inasuasua kutokana na viongozi kushindwa kuwashirikisha ipasavyo  wananchi kwenye miradi ambayo nguvu zao zinahitajika.

 

"Miradi mingi tuliyoitembelea iko katika hatua nzuri ya ukamilishaji isipokuwa michache hasa Ile inayohitaji nguvu za wananchi hapa naona kuna uzembe hasa kwa viongozi kwenye maeneo husika ambao ndiyo wasimamizi wa miradi na tumetoa maelekezo kwenye miradi hiyo tunataka ikamilike kwa muda ambao tume uweka leo kama tulivyoagiza Ili itumike," amesema.

 

Amesema kuwa katika Ujenzi wa miradi ya Serikali hakuna ubabaishaji na kusisitiza milango ya mbao inayowekwa kwenye majengo hayo iwe imara itakayodumu  kwa muda mrefu huku akiagiza kuondolewa kwa milango katika nyumba ya  Mganga katika zahanati ya kijiji cha Nguliguli.

 

"Katika miradi ya Serikali hakuna masuala ya ubabaishaji tunahitaji kuweka vitu vyenye ubora kwenye majengo yetu nimeona hii milango mnayoweka haifai kabisa kwenye majengo ya Serikali hivyo Ile milango kwenye nyumba ya Mganga wa zahanati ya kijiji cha Nguliguli iondolewe yote iwekwe mingine," amesema.

 

Pia ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi juu ya mchakato wa manunuzi ya milango ya mbao katika bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Binza ambapo mlango mmoja umenunuliwa kwa Sh milioni moja.

 

Aidha amewataka wasimamizi wa miradi kuandaa taarifa ambayo inayoonyesha matumizi ya fedha ambazo zilitolewa kwa ajili ya uendeshaji wa kila mradi pamoja na shughuli zilizopaswa kufanyika na kuitembelea mara kwa mara ili kubaini changamoto zinazokwamisha miradi hiyo kutokamilika kwa wakati ili kuweza kuzitatua kwa wakati.

 

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Vivian Chirstian amesema kuwa  mapungufu yote yaliyojitokeza katika baadhi ya miradi waliyoitembelea watayafanyia kazi ili kuhakikisha inakamilika na kuanza kutumika kwa manufaa ya wananchi.

 

Miradi ambayo imetembelewa ni  Ukarabati wa miundombinu katika shule ya msingi Shanwa,Ujenzi wa bweni moja la Wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Binza,Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Mwawayi na Ujenzi wa matundu 24 ya vyoo katika shule ya sekondari ya Binza.

 

Miradi mingine ni pamoja Ujenzi wa shule mpya ya msingi katika kijiji cha Mwabaraturu,Ujenzi wa nyumba ya daktari katika zahanati ya kijiji cha Nguliguli na Zananati na Kijiji Cha Kizungu, Upanuzi wa majengo katika Zahanati ya Kijiji Cha Nguliguli.

 

Pia miradi mingine ambayo imetembelewa na kukaguliwa ni pamoja na Ujenzi wa Vituo vya Afya vya Badi, Shishiyu, na Zebeya.

 

MWISHO.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم