TAKUKURU Rafiki yaanza kuwafikia wananchi Kata kwa Kata.

                 TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

 


Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Simiyu Fauzati Rajabu, akizungumza na wananchi wa kata ya Kasoli (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa TAKUKURU Rafiki uliofanyika shule ya msingi Dk. Otto.


 Wananchi wa Kata ya Kasoli wakiwa kwenye semina maalumu ya kuzindua mfumo wa TAKUKURU Rafiki uliozinduliwa kwenye kata hiyo.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeanzisha Programu ya TAKUKURU Rafiki ili kuongeza ushiriki wa kila mwananchi katika kukabiliana na tatizo la Rushwa katika utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 

Akizungumza juzi kwenye uzinduzi wa program hiyo uliofanyika kata ya Kasoli wilayani Bariadi, Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Simiyu Fauzati Rajabu alisema wamezindua mpango huo ili kuzuia vitendo vya rushwa katika sehemu za kutolea, kupokea huduma na kwenye miradi ya maendeleo.

 

Amesema serikali inajitahidi kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika miradi ya kipaumbele kwenye sekta za Afya, Elimu, Maji, Nishati, Barabara na Ardhi ambapo wamekuja na mpango wa TAKUKURU rafiki.

 

‘’Mpango huu ni mahususi kwa ajili ya kuwasogeza karibu wananchi kwa ajili ya kuzuia vitendo vya rushwa, katika mpango huu lazima tuainishe kero tulizonazo ili kumaliza vitendo vya ruwasha…tusiposhughulikia kero zilizopo kuna uwezekano mkubwa wa vitendo vya rushwa kutokea’’ amesema Afisa huyo.

 

Amesema Programu ya TAKUKURU rafiki inatarajiwa kuchangia kukuza ustawi wa utawala bora kwa kuzuia vitendo vya rushwa visitokee katika utoaji wa huduma kwa umma, kuokoa upotevu wa fedha za umma.

 

Amefafanua kuwa mpango huo umeanza kutekelezwa nchi nzima tangu ulipozinduliwa Februari mosi mwaka huu, na katika wilaya ya Bariadi mpango huo umezinduliwa kata ya Kasoli.

 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kasoli Mayala Lukas ameipongeza TAKUKURU kwa kuja na mfumo wa TAKUKURU Rafiki ambao utachochea miradi ya maendeleo kutekelezwa kwa ubora.

 

Amesema mpango huo unawajenga wananchi kusimamia na kutoa ushirikiano baina yao na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za ubadhirifu wowote wa miradi ya maendeleo unaofanywa chini ya kiwango wakidhani wamepokea rushwa.

 

Emmanuel Ndiganya mkazi wa Kasoli ameipongeza TAKUKURU kuwafikia wananchi vijijini ili kujionea changamoto zinazowakabili na kuwaweza kuzitatua kwa haraka na pia mpango huo utaimarisha mahusiano baina ya wananchi na taasisi hiyo.

 

Ameongeza kuwa awali elimu ya mapambano ya Rushwa ilikuwa haijawafikia ipasavyo, lakini kupitia mpango huo wananchi wengi wataelimika na kutoa ushirikiano wanapoona viashiria vya vitendo vya rushwa.

 

MWISHO.

 

 Wananchi wa Kata ya Kasoli wakiwa kwenye semina maalumu ya kuzindua mfumo wa TAKUKURU Rafiki uliofanyika shule ya msingi Dk. Otto Kasoli.

 

Wananchi wa Kata ya Kasoli wakiwa kwenye semina maalumu ya kuzindua mfumo wa TAKUKURU Rafiki uliozindiliwa kwenye kata hiyo.

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم