Uwanja wa Mkapa wapigwa 'Stop'


Uwanja wa Mkapa.


Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limeshauri Uwanja wa Benjamini Mkapa uliopo jijini Dar es Salaam kutotumika kwenye mechi zao kwa kile kilichoelezwa kuwa umeharibika eneo la kuchezea (pitch), ambapo sasa utafungwa kwa mwezi mmoja kupisha marekebisho.

Hivyo basi, baada ya mechi ya leo Jumatano ya Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na KMC, itakayochezwa kuanzia saa 10:00 jionib uwanja huo utafungwa.

Kwa mujibu wa matumizi ya uwanja huo, unapaswa kutumika mara tatu kwa wiki lakini hadi leo itakuwa ni mara ya nne kinyume na matumizi ya uwanja huo ambao hata kabla ya hapo ulilalamikiwa kutokuwa katika hali nzuri hasa eneo la kuchezea (pitch), kwani matumizi yamekuwa makubwa.

Tangu Jumamosi iliyopita, uwanja huo ulianza kutumika na Simba walipoikaribisha Raja Casablanca mechi yao ya pili ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifungwa mabao 3-0.

Siku iliyofuata, Yanga nao waliikaribisha TP Mazembe mechi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika ikishinda mabao 3-1.

Baada ya mechi hizo za CAF, jana Jumatatu kulikuwa na mechi ya Ligi Kuu Bara, Simba ilicheza na Azam usiku kuanzia saa 1:00 na leo ni KMC na Yanga ambapo zitakuwa zimebaki siku tatu kufikisha wiki moja, hivyo matumizi yamezidi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Uwanja huo, Salum Mtumbuka alisema kuwa baada ya mechi mbili za CAF zilizochezwa wikiendi iliyopita walikutana na maofisa hao ambao waliwapa maelekezo namna ya kufanya marekebisho hasa eneo la kuchezea.

"Tulikubaliana kwa pamoja na Caf kwamba wakati marekebisho yanaendelea ambayo yatachukua muda wa mwezi mmoja, mechi zitakazochezwa hapo hapo labda ni zile za kimataifa za CAF na timu ya Taifa, mechi zingine za ligi kuu wanaotumia uwanja huu watatafuta viwanja vingine hata Uhuru upo.

"Simba na Yanga ndiyo wanaotumia huu uwanja kama uwanja wao wa nyumbani, ila ndani ya kipindi cha marekebisho haya hawatatumia mechi zao za Ligi Kuu kwenye uwanja huu, tunawapa Uwanja wa Uhuru ama watakavyoona nao," alisema na kuongeza;

"Matumizi ya uwanja huu ni kwamba ndani ya wiki moja zinatakiwa kuchezwa mechi tatu tu kwa maana ya siku tatu, lakini sasa umetumika sana kinyume na matumizi ya uwanja, tumeacha hizi mechi mbili za ligi zichezwe ambapo kesho (leo) Yanga na KMC wakicheza tunaufunga."
 
 
SOURCE- Mwanaspoti.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post