Waziri aomba michomoko irejeshwe Simiyu.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi Mashimba Ndaki.

 

Na Derick Milton, Bariadi.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi Mkoani Simiyu Mashimba Ndaki ameuomba uongozi wa Mkoa huo, kutafakari upya juu ya katazo lake la Magari madogo (Michomoko) kutofanya kazi ya kusafirisha abiria ndani ya mkoa huo.


Kauli hiyo ya Waziri nakuja zikiwa zimepita wiki mbili tangu Chama cha mapinduzi (CCM) mkoani huo, kuutaka pia uongozi wa Mkoa kutafakari upya katazo hilo kwani limeadhiri ajira za vijana wengi.


 Julai 13, 2022 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo David Kafulila, aliweka zuio la magari hayo kufanya kazi ya kusafirisha abiria ndani ya mkoa huo, hiyo ni baada ya kutokea ajali mbili mfulululizo na kusababisha vifo vya watu 10 na majeruhi 17 ndani ya siku 12.


Wakati akipiga marufuku magari hayo, Kafulila alisema kuwa yalikuwa yakifanya kazi kinyume cha utaratibu wa leseni zao, huku akibainisha kuwa yalikuwa yakipakia abiria hadi 11 wakati uwezo wake ni abiria watano.


Jana kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) Waziri ndani akichangia mada mbalimbali, aliomba uongozi wa mkoa kukaa kwa mara nyingine na kutafakari zuio hilo kama bado lina tija kwa ajira za vijana au hapana.


Ndaki alisema kuwa magari hayo yalikuwa yameajiri vijana wengi, ambao kwa sasa wamebaki bila ajira baada ya marufuku hiyo, huku akitaka kutafutwa njia mbadala ya kuzuia ajali lakini magari hayo yaendeleee kufanya kazi.


Alisema kuwa serikali inazo njia nyingi na zenye kuwezesha kuzuia ajali za mara kwa mara Barabarani kutokana na kuwa na vyombo vingi vya kupambana na jambo hilo.


“ Hata tukiangalia kwa sasa ajali bado zinaendelea kutokea, mimi nafikiri tunaweza kukaa meza moja tena na wahusika wa magari haya, tukatafuta njia sahihi ya kuzuia ajali na siyo kuzuia wafanye kazi” alisema Ndaki….


“ Kuendelea kuzuia magari haya vijana wengi wanaendelea kuteseka uko mitaani, hawana ajira na hii ndiyo ilikuwa ajira yao, walijiajiri wenyewe, na kazi hii ilikuwa halali siyo kwamba ilikuwa haramu, kama ilikuwa halali na wana leseni, wanalipia mapato kwanini wazuiwe?”

Alisema kuwa ni vyema yakawepo makubaliano kwa pande zote husika, ya jinsi ya kukomesha ajali na kuwekeana masharti ya ubebaji abiria ili vijana waendelee kufanya kazi na kujiingizia kipato.


Akizungumzia jambo hilo Mkuu wa Mkoa Dkt. Yahya Nawanda ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho alisema kuwa, hata yeye alikuta zuio hilo hivyo atakaa na kamati yake ya ulinzi na usalama kuweza kulijadili upya jambo hilo.


Nawanda alisema kuwa hadi kufikia uhamuzi huo, jambo hilo lilianzia kwenye kamati hiyo, hivyo lazima alirudishe uko uko kujadiliwa upya kama ambavyo Waziri ameshauli kwani ndicho chombo chake kikuu cha kumshauri.


“ Chombo changu kikubwa cha kunishauli ni kamati ya ulinzi na usalama, Mheshimiwa Waziri tumepokea ushauli wako na tutakwenda kuufanyia kazi na kamati yangu, kisha tutakuja na majibu” alisema Nawanda.

 

MWISHO.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post