Mmoja wa akina mama ambaye mtoto wake amelazwa katika hospitali ya Mji wa Bariadi (Somanda) kutokana na mtoto wake kuwa na Utapiamlo.
MAAFISA na Askari wanawake kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) wakisikiliza na kumfariji mmoja wa wakina mama aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya Somanda mjini Bariadi kutoka na mtoto wake kuwa na tatizo la Utapiamlo.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
KUELEKEA Maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani, Maaskari wanawake kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) wameshiriki maadhimisho hayo kwa kutoa misaada ya kibinadamu na kutembela wodi ya watoto wenye Utapiamlo katika hospitali ya Somanda iliyopo mjini Bariadi.
Akizungumza leo mara baada ya kukabidhi misaada hiyo, Kamanda wa Uhifadhi wa TAWA kanda ya ziwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Gisela Kimario alisema wameungana kuwafariji akina mama ambao wamelazwa katika hospitali ya Mji wa Bariadi kuelekea siku ya Wanawake duniani.
Amesema Mamlaka hiyo ni sehemu ya jamii na wanatambua kuwa Mwanamke anapouguliwa au kuumwa jamii au familia inapata pigo, ambapo askari na maafisa wa mamlaka hiyo wanajua changamoto za kuugua na kuuguliwa.
‘’Tumeona tushiriki upendo huu kuelekea siku ya wanawake duniani ili kuwafariji wakina mama wenzetu, tunaamini watoto wanaoumwa ni taifa la kesho na wahifadhi wa kesho’’ amesema Kamanda Kimario.
Ameeleza kuwa wamefanya tukio hilo ili kudhibitisha kuwa ni sehemu ya jamii na kwamba wanafanya uhifadhi kwa manufaa ya jamii na Mamkala hiyo imekuwa ikichangia shughuli za maendeleo katika sekta za elimu, afya na maji.
Amesema kutokana na fedha zinazopatika katika uhifadhi, zimekuwa zinakwenda kuchangia maendeleo katika jamii kwenye Nyanja za elimu kwa kujenga madarasa na nyumba za walimu, afya kwa kujenga zahanati, vifaa tiba pamoja na visima vya maji.
‘’Waupende uhifadhi kwa sababu una faida kwa jamii, kupenda uhifadhi ni kuzuia ujangili sababu ujangili unamnufaisha mtu mmoja…lakini uhifadhi unafaidisha jamii yote, tunaitaka jamii iungane na TAWA katika uhifadhi’’ amesema.
Kwa upande wake Winfrida Stanslaus kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori (TAWA) amesema wametembelea hospitali ya Somanda kwa sababu inapakana na Pori na Akiba la Maswa.
Aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kupinga ujangili kwa sababu wanaume wengi wanafanya ujangili na wakikamatwa, familia zinatunzwa na wanawake.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Somanda, Dk. Rosemary Mushi amewapongeza maaskari na maofisa wanawake kwa kumuunga mkono Rais Samia na kutoa msaada kwa watoto wenye matatizo ya utapiamlo.
Amesema wagonjwa wenye tatizo la utapiamlo wana uhitaji mkubwa na uangalizi maalumu ambapo Maaskari hao wameleta mablanketi ya kuwakinga na baridi, sabuni na mafuta kama sehemu ya matibabu.
‘’hali ya utapiamlo katika hospitali yetu ni kubwa kidogo kwa sababu hospitali hiyo ni kituo cha Rufaa kwa wilaya ya Bariadi na Itilima, kwa mwezi tunahudumia wagonjwa 40 mpaka 50…tunakaa nao kwa mwezi mmoja, tunawapa elimu na chakula cha lishe kwa gharama za serikali’’ amesema.
Naye Kija Keleja kutoka kijiji cha Itubukilo amesema alimfikisha mtoto wake katika hospitali hiyo akikutwa na tatizo la utapiamlo, hali iliyomfanya kushindwa kutembea wala kukaa.
Kija Liku kutoka kijiji cha Nanga wilaya ya Itilima amewapongeza maaskari hayo wanawake kwa kutoa msaada kwa wagonjwa ambapo alisema mtoto wake alikuwa anatapika, kukohoa na kuharisha na alipopimwa alikutwa na tatizo la utapiamlo.
MWISHO.
إرسال تعليق