TARI yasisitiza wakulima mazao yanayostahimili ukame.

 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahya Nawanda, akiwagawa mbegu za kisasa za viazi kwa wakulima walioshiriki siku ya Mkulima Shambani katika kituo cha umahili cha usambazaji wa teknologia ya mbegu za kisasa TARI Nyakabindi kilichopo Mkoani humo (kulia) Ofisa Mfawidhi wa kituo hicho Isabera Mrema.



Na Derick Milton, Nyakabindi.


Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) imewasisitiza wakulima katika kipindi hiki ambacho Mamlaka ya hali ya hewa nchini imetangaza kuwepo kwa mvua chache zitakazonyesha, kutumia mbegu zinazozalishwa na kituo hicho ambazo zinastahimili ukame.


Aidha wakulima wametakiwa kuzitumia mvua hizo kwa manufaa, kwa kutumia teknologia zinazoendana na hali ya hewa hiyo ambazo nyingi zinapatika kwenye vituo vyake vya umahili vya usambazaji teknologia za kisasa.


Wito huo umetolewa na Dkt. George Sonda Mratibu wa uhaulishaji wa teknologia kutoka TARI ukiriguru mkoani Mwanza, wakati akizungumza na wakulima mkoani Simiyu kwenye kituo cha umahili cha usambazaji wa teknologia za kisasa TARI Nyakabindi kwenye siku ya mkulima.


Dkt. Sonda amesema kuwa ni wakati sasa wakulima kutumia mvua hizi chache kwa umakini, kwa kutumia teknologia za kisasa ili waweze kuzalisha kwa tija, ikiwemo kupanda mazao kama mtama, mihogo ambayo yanayostahimili ukame.


“ Tunawasisitiza wakulima na kuwashauri sana katika hali hii ya mvua chache zilizotangazwa, tutumie vituo vyetu vya TARI kupata teknologia ambazo zitatusaidia kuzalisha kwa tija,” amesema Dkt. Sonda…..


“ Vituo vyetu vyote kikiwemo hiki cha Nyakabindi, vina teknologia za kutosha, tunawashauri wakulima watumie hivi vituo kuja kuchukua mbegu bora ambazo zinaweza kupambana na ukame, magonjwa, lakini zenye mavuno mengi,” aliongeza Dk. Sonda.


Mtafiti kutoka TARI tumbi Mkoani Tabora Martha Ndelemba, amewashauri wakulima kwenye kipindi hiki kulima zao la mtama kwa kutumia mbegu bora aina ya TARISO TWO inayastahimili ukame na mazao yake ni mengi.


“ Kwa sasa TARI tuna mbegu bora ya zao la Mtama, inaitwa TARISO TWO, wakulima tunawashauri kwa kipindi hiki watumie mbegu hii, inastahimili ukame, mazao yake ni mengi lakini pia ustahimili mashambulizi ya magonjwa” amesema Ndelemba.


Ofisa Mfawidhi wa kituo hicho cha Nyakabindi Isabela Mrema amesema tangu kituo kianzishwe toka mwaka 2021, jumla ya wakulima 3,121 wanawake wakiwa 750 na wanaume 2,371 wamepewa mafunzo ya teknologia za kisasa.


Isabela amesema kuwa mwitikio wa wakulima kuja kwenye kituo hicho umekuwa mkubwa, ikiwemo vijana kutembelea kituo hicho kwa ajili ya kujifunza teknologia za kisasa na kuchukua mbegu bora.


MWISHO.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم