CHIFU Isucha wa Pili wa Dutwa kutoka Kabila la Wasukuma (mwenye kofia nyekundu) akiwa na baadhi ya wasaidizi wake, katika moja ya Pango la Wafalme katika mlima Dutwa, pango ambalo lililotumiwa kama makazi ya wafalme karne ya 16.
Na COSTANTINE MATHIAS.
MUSHUDA Balina alikuwa Mtemi wa uchifu wa Dutwa katika Kabila la Wasukuma, alipofariki, alizikwa kwa kutenganishwa kichwa na kiwiliwili, mwanzoni mwa karne ya 20 katika miaka 1900.
Ikumbukwe kuwa, huko nyuma hapakuwa na usafiri, lakini pia Mtemi alikuwa akisafiri na watu wengi kwa ajili ya kumbeba begani kwa kutumia machela (Lugega), hivyo hata wakati anapelekwa kwenye matibabu alibebwa kwenye machela.
Chifu Isucha wa pili wa Dutwa aliyetawazwa mwaka 2019, anasema Mtemi Mushuda Balina alikuwa babu yake ambaye aliwataka machifu wa kabila la Wasukuma kuendelea mila na tamaduni za Uchifu wa Dutwa.
Anasema katika utawala wake, Mtemi Balina alitawala kwa miaka sita, baada ya mvua ikagoma kunyesha na wananchi wakamkataa kuwa hawasaidii kupata mvua ili waivishe mazao ya chakula.
‘’Baada ya kukataliwa na wananchi alikwenda kuishi kijiji cha Nyakabindi, lakini baadae wakamfuata kwa ajili ya kuendelea kutawala, akatawala tena kwa miaka sita’’ anasimulia Chifu Isucha wa pili.
Anaongeza kuwa, wakati wa Utawala wa Chifu, Jamii ilikuwa inahitaji kupata mvua ya kutosha ili kupata mazao ya chakula, kupiga vita magonjwa ya mlipuko pamoja na kuzuia Vita na uvamizi kwenye himaya ya Chifu.
Anasema akiwa madarakani aliugua na kupelekwa hospitali ya Sekou Toure iliyoko Mkoani Mwanza, kwa ajili ya matibabu lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia na walikuwa wanatembea kwa miguu sababu hapakuwa na usafiri.
Anaendelea kusema, baada ya kufariki, walimkata kichwa ili wasafirishe kirahisi na kuacha kiwiliwili huko Mwanza, na walikuja kuzika kichwa pekee yake eneo la Utemi lililoko Dutwa.
Na baada ya mazishi, Padri mmoja wa Kanisa Katoliki alipata taarifa kuwa Mtemi Mushuda amezikwa kichwa pekee yake, akatoa gari yake kwa ajili ya kufuata mwili nao ukaja kuzikwa sehemu yake.
‘’alikatwa kichwa ili warahishe kumsafirisha na wakazika kichwa, padre wa Kanisa Katoliki aliuliza mwili wa Chifu uko wapi, akajibiwa tumeuacha…aliwasha gari akaufuata, ndio maana huyu babu yangu ana makaburi mawili, kaburi la kichwa na kaburi la mwili’’ alisema Chifu Isucha.
Baada ya kifo cha Mtemi Mushuda.
Mtemi Isucha wa Pili, anaendelea kusimuliwa kuwa baada ya kifo cha Mtemi Mushuda, alitawala Mtemi Kisula kwa muda wa miaka 12, naye akafukuzwa na waingereza wakati wa vita ya kwanza ya dunia kutokana na kuwa na urafiki wa wajerumani ambao alikuwa anawaficha Ikulu.
Anasema walipotawala Waingereza, Mtemi Kisula alikimbila Nasa kujificha na akaletwa mtemi kutoka Nasa aliyekuwa anaitwa Shimba Kapongo ili kutawala utemi wa Dutwa, alitawala kwa muda wa miaka mitano.
Mtemi Kapongo alinyweshwa sumu na wana ukoo wa Uchifu wa Dutwa akafariki kutokana na kutokubaliwa na uchifu wa Dutwa kwani alikuwa hatokani na jamii ya ukoo ule.
Alitawala Mtemi Ileme kwa muda wa miaka 15 na mwaka 1940 alifariki dunia, baada ya kufariki Mtemi Ileme, akatawala mtoto wake aliyekuwa anaitwa Buyunge Ileme.
Mtemi Buyunge alitawala kwa miaka mitano na baadae aliuwawa na wakoloni kutokana na kumpiga bwana shamba aliyekuwa akilazimisha watu kulima zao la pamba ambalo yeye mtemi alidai haliwezi kuliwa na watu wake.
Kufuata Mila, Desturi na Kujenga Ikulu ya Dutwa.
Mtemi Isucha wa Pili anasema lengo la Utemi ni kuendeleza mila za kiafrika ili kuhakikisha waafrika wanafuata mila zao na kuacha mila kigeni ambazo zingine zinapotosha.
Anaitaka jamii kuafata mila na desturi zenye maadili, heshima na staha katika kwa watu wote ili kuwa na kizazi kizuri chenye kuheshimu kila mmoja kwa rika na umri.
Lengo lake lingine ni kujenga Ikulu ya Utemi wa Dutwa ili kuwa kituo cha Utalii kwa sababu nchi ya Tanzania ina machifu wengi na kila chifu ana ngome yake ambazo ni fursa katika utalii.
‘’sisi tumetawala miaka 500 hapa Dutwa, tumeanza kujenga jumba la makumbusho, ili watu waweze kuja kujifunza historia kwa sababu Utemi wa Dutwa ni sehemu ya Himaya za kale na kuhifadhi mazingira’’ alisema Chifu Isucha.
Anasema katika eneo la Dutwa kuna makumbusho ya aina mbalimbali ikiwemo Pango la Kifalme ambalo wafalme walikuwa wanaisha, kuna visima vya maji vya maajabu, historia ya machifu pamoja na kaburi la Mtemi Mushuda Balina aliyezikwa kwa kutenganishwa kichwa na kiwiliwili.
Anaongeza kuwa ‘’Mimi ni chifu wa 29 hapa Dutwa, waliotangulia ni wengi na makaburi yao yako hapa, kuna simulizi nyingi kwa miaka 500 tangu karne ya 16…vivutio ni vingi sana’’
Anasema kuna haja ya kupanua Utalii wa Kihistoria sababu kuna nchi zingine hazina hata wanyama lakini wanafanya utalii na wanapata fedha za kigeni ikiwemo nchi ya Misri.
Anaiomba serikali kuwekeza katika Utalii wa kihistoria kwa kila utemi ili kuongeza mchango wa pato la Taifa kwenye utalii kama zinavyofanya nchi za Uingereza kwenye Makasri yao ya kifamle.
Anafafanua kuwa Machifu wanamuunga Mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika Utawala wake kwa kuendelea kuipigania nchi ya Tanzania ili kukuza uchumi kupitia Utalii.
‘’Rais Samia ni Chifu mwenzetu, tulimsimika pale Mwanza na kumwita jina la Hangaya maana yake Nyota ya asubuhi inayong’aa…Rais Samia naye ameng’aa na anaendelea kung’ara’’ anasema Chifu Isucha wa Pili.
Nengelo Mdaha mkazi wa Dutwa anasema Chifu anatakiwa asimamie masuala ya kilimo, upatikanaji wa mvua pamoja na kuendeleza ngoma za asili ili wasukuma waendeleze utamaduni wao baada ya mavuno.
Anasema Chifu anatakiwa kuwakumbushia watu Mila, Desturi na Utamaduni wa eneo husika kwa kuzingatia kuwa jamii ya sasa imeacha mila na desturi na kuiga mambo ya kisasa.
Jackson Wishi anasema wanaendeleza makumbusho hayo ili yaweze kuwa mfano kama ilivyo eneo la Makumbusho ya Bujora mkoani Mwanza, ambapo jamii na watalii wataweza kujifunza mambo mbalimbali ya utamaduni.
Anaongeza kuwa, katika jamii ya sasa mila zimeacha na maadili yameporomoka sana sababu watoto wadogo wanavaa nguzo sizizo kuwa na staha na zisizokuwa za kitamaduni.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment