Jengo la Zahanati ya Kijiji Cha Igwata ambalo limepatiwa vifaa vya Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki Kwa ajili ya kuezekwa Jengo lote.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji Cha Ikungu waliojitokeza kumsililiza Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki (hayupo pichani) kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Na Samwel Mwanga, Maswa.
MBUNGE wa Jimbo la Maswa Magharibi mkoa wa Simiyu, Mashimba Ndaki amefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kuchangia zaidi ya Shilingi mil. 39 kwa ajili ya kukamilisha Ujenzi wa Zahanati tatu zilizopo katika jimbo hilo.
Zahanati ambazo zimechangiwa kila moja vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 13 ambazo zinaendelea na Ujenzi ni Zahanati katika Kijiji cha Ikungu,Kijiji cha Kidema na Kijiji cha Igwata.
Zahanati hizo kila moja imepewa mabati, mbao na misumari kwa ajili ya kuezeka mamboma hayo ambayo yote yamejengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Mbunge huyo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na Wananchi wa vijiji hivyo wakati akikabidhi vifaa hivyo vya ujenzi, Mashimba amesema kuwa ni vizuri Viongozi wa serikali katika vijiji hivyo na Kata kuhakikisha wanasimamia shughuli za kuezeka mabati kwenye majengo hayo ya zahanati kwa wakati na ubora kwani vifaa vilivyotolewa vinatosheleza.
Pamoja na kuwataka viongozi hao kusimamia ujenzi huo amesema kuwa atachukua hatua kali kwa kiongozi yeyote wa serikali ya Kijiji ama Kata ambaye atatumia vibaya madaraka yake kuhujumu vifaa vilivyotolewa kwa ajili ya kukamilisha zahanati hizo.
"Nimetoa kwa kila zahanati mabati,mbao na misumari ya kutosha ajili ya kumaliza kazi ya kupaua na kuezeka hivyo vifaa hivyo visihujumiwe na kiongozi yeyote wa ngazi yoyote iwe Kijiji au Kata huyo akibainika nitamshughulikia,"amesema.
Amesema kuwa akiwa Mbunge wa jimbo hilo ameamua kutekeleza ahadi yake hiyo aliyoitoa kwa wananchi akiwaunga mkono juhudi zao za maendeleo za ujenzi wa zahanati hizo.
"Nimeona ni vema kuwapunguzia makali wananchi wa jimbo langu kwenye maeneo ambayo mmejenga hizi zahanati kama nilivyowahaidi na fedha hizo nimezitoa kupitia mfuko wa Jimbo,"amesema.
Mashimba amesema katika Zahanati ya Ikungu ametoa mabati 230,mbao 740 na misumari vyote vikiwa na thamani ya Sh 13,108,000,Zahanati ya Kidema ametoa mabati 200,mbao 485 na misumari vyenye thamani ya Sh 13,180,000 na Zahanati ya Igwata ametoa mabati 200,mbao 600 na misumari vyote vikiwa na thamani ya Sh 13,800,000.
Amesema kuwa hakuna mwananchi yeyote atakayechangishwa wakati wa umaliziaji wa Ujenzi wa Zahanati hizo hivyo kwa sasa wajipange kuanza Kujenga nyumba za Waganga katika kila zahanati nyumba moja.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Adorat Mpolo pamoja na kuwashukuru Wananchi wa vijiji kwa ujenzi wa zahanati hizo Kwa kushirikiana na Mbunge huyo amehaidi kuziingiza kwenye bajeti Ili Kila zahanati iweze kupatiwa kiasi cha Sh Milioni 50 kutoka serikalini kwa ajili ya kuvimalizia Ili viweze kutoa huduma kwa Wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Wilaya ya Maswa,Onesmo Makota amesema kuwa amesema kinachofanywa na Mbunge huyo ni kutekeleza ila ya CCM katika sekta ya Afya.
Amesema kuwa serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu imekuwa ikiweka mbele suala la Afya kwa wananchi wake ndiyo maana zahanati na Vituo vya Afya vinajengwa kwa kasi na kupatiwa vifaa tiba pamoja na wataalam wa Afya.
"Tumeamua kusogeza huduma za Afya kwa wananchi Ili kuwanusuru wananchi wetu hasa wakinamama wajawazito ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu hasa maeneo ya vijijini kufuata huduma ya kujifungua na wengine kwa bahati mbaya hujifungulia barabarani hivyo zahanati hizi zikikamilika kwenye maeneo hayo watapunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya,"amesema.
MWISHO.
Post a Comment