Mashimba achangia Saruji mifuko 450 Ujenzi wa Miundombinu ya Elimu na Afya Maswa Magharibi.

 

 MBUNGE wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akikabidhi mfuko wa saruji kwa Uongozi wa Kata ya Mwamashimba kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Zahanati ya Buyubi akitoa mifuko100.

 

MBUNGE wa Jimbo la Maswa Magharibi Mashimba Ndaki (mwenye shati la kitenge) akiwakabidhi Viongozi wa Kijiji Cha Ilobi mifuko ya saruji kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati

Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki akichimba msingi kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji Cha Ilobi.


 Baadhi ya Viongozi wa Kijiji Cha Mwaliga wakiwa eneo ambalo itajengwa Zahanati ya Kijiji Cha Mwaliga na aliye mbele ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki.

 

 


 

Na Samwel Mwanga, Maswa.

 

MBUNGE wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki ametoa mifuko 450 ya saruji  yenye thamani ya zaidi ya Shilingi mil. 9 kwa ajili ya kuunga  mkono jitihada za wananchi katika Ujenzi wa miradi katika sekta ya elimu na afya katika jimbo hilo.

 

Saruji hiyo itatumika kuanza Ujenzi wa miundombinu ya Shule ya sekondari Bukigi, Kituo cha Afya Zanzui,  Zahanati ya Ilobi, Zahanati ya Mwaliga na Zahanati ya Buyubi.

 

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati akikabidhi saruji hiyo alisema kuwa katika kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo anataka kuweka alama katika kila eneo ikiwa ni sehemu ya utumishi wake kwao

 

Mbunge Mashimba alisema kuwa moja ya vipaumbele vyake ni elimu na afya ndiyo maana nguvu kubwa ameielekeza huko kwa sababu Elimu ndiyo msingi wa maisha na ukiwa na Afya njema utashiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo za Taifa na za binafsi.

 

 Amekabidhi mifuko ya saruji  150 kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Shule ya sekondari Bukigi katika Kata ya Malampaka, Mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya Ujenzi wa kituo cha Afya Zanzui katika Kata ya Zanzui  na mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati katika Kijiji Cha Buyubi katika Kata ya Mwamashimba.

 

Pia amekabidhi mifuko 50 ya saruji katika Kijiji Cha Mwaliga katika Kata ya Shishiyu kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Zahanati na mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Zahanati katika Kijiji Cha Ilobi katika Kata ya Jija.

 

“Nilifanya ziara katika vijiji vya kata hizo nikaona wananchi wanavyojitoa katika kuanzisha miradi ya maendeleo katika  sekta ya Elimu na Afya mimi kama mbunge wao nikaamua kuwaunga mkono kwa kuchangia mifuko hiyo ya saruji na watakapojenga hayo majengo na kufikia hatua ya kuezeka bati kazi hiyo nitaifanya mimi maana nitaleta mbao,mabati na misumari ya kutosheleza majengo yote,” alisema Mashimba.

 

Alisema kuwa ni vizuri viongozi wa serikali katika maeneo hayo ambayo ametoa saruji hiyo wakasimamia kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

 

Pia amewahaidi wananchi kuwa pindi watakapokamilisha Ujenzi wa majengo hayo na kufikia hatua ya kuezeka atatoa vifaa vyote vya Ujenzi ambavyo ni mabati,mbao na misumari.

 

'Hawa Wananchi wakishajenga haya maboma mie kazi yangu  itakuwa ni kuezeka maana nitatoa vifaa vyote ambavyo ni mbao,mabati na misumari,"alisema.

 

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Maswa, Onesmo Makota alisema kuwa anachokifanya mbunge huyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

 

Alisema kuwa CCM ilihaidi mambo mengi katika sekta mbalimbali zikiwemo Elimu, Afya, Maji, Barabara ambapo kwa wameanza kutekeleza ili ikifika mwaka 2025 kwenye uchaguzi mkuu wananchi watakapohoji waonyeshwe yaliyoyafanywa kupitia viongozi wa CCM.

 

MWISHO.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم