Mpango wa Matumizi Bora ya ardhi Watambulishwa Maswa.


Afisa Mipango Miji Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Aristides Mulokozi akiwakilisha Mpango Kiunzi wa matumizi ya Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa kwenye Baraza la Madiwani.
 
 

Baadhi ya madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu wakifuatilia juu ya mpango wa Kiunzi wa matumizi bora ya Ardhi katika Halmashauri ya wilaya hiyo.

 

 

Na Samwel Mwanga, Maswa.

 

SERIKALI kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imetambulisha Mradi wa Mpango Kiunzi wa Matumizi Bora ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu ambao unatarajia kuondoa migogoro ya Ardhi kati ya wananchi na hifadhi za wanyamapori.

 

Pia mpango huo unatarajia kutoa  hati miliki za kimila zaidi ya 100,000 zikitarajia kutolewa kwa wananchi wa wilaya hiyo.

 

Akitambulisha mpango huo mbele ya madiwani wa Halmashauri hiyo, Afisa Mipango Miji Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Aristides Mulokozi anasema mpango huo ni nyenzo kisheria ya kutatua changamoto kwa kuzuia uharibifu wa ardhi na rasilimali zake  na kulinda maeneo ya uwekezaji.

 

Amesema kuwa mpango huo utasimamia uhamaji wa watu na mifugo, uhifadhi wa bioanuwai na kwamba  unasimamia kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali za ardhi.

 

"Mpango huu ni mzuri utawezesha ufanisi wa utawala wa matumizi ya ardhi,wamiliki na watumiaji wa ardhi kutumia ardhi yao kwa ufanisi, kumwezesha uchambuzi na ulinganifu wa taarifa za kijamii na kiuchumi dhidi ya taarifa za kijiografia," amesema.

 

Amesema kuwa Halmashauri hiyo ilipendekezwa kutekeleza Mpango huu Ili kuhakikisha kuwa kuna usimamizi endelevu wa matumizi ya rasilimali ardhi kwa kipindi cha miaka 20 ijayo kutokana na kukua kwa sekta za miundombinu.

 

Naye Afisa Ardhi wa Wilaya ya Maswa, Vivian Crisitian anasema mpango huo umekuja wakati sahihi kwani unakwenda kuondoa kabisa migogoro ya ardhi katika Wilaya hiyo.

 

"Mpango huu ndiyo mwarobaini wa kuondoa migogoro ya ardhi katika wilaya yetu kwani utaweka matumizi bora ya ardhi katika wilaya yetu hasa maeneo ya vijijini,"

 

"Pia hati za kimila za kumiliki ardhi zitaongezeka kufikia 100,000 kukinganisha na sasa ambazo ziko 2040 na hizi zitawasaidia wananchi kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha na hata kutoa dhamana kwa watu mahakamani na kituo cha polisi,"amesema 

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Paul Maige ameshukuru Rais, Dkt Samia Suluhu kwa kumwezesha wilaya hiyo kuwa miongoni mwa wilaya sita hapa nchini kutekeleza mpango huo.

 

Mpango huo unatekelezwa katika wilaya sita hapa nchini zikiwemo wilaya za, Mbinga, Songwe, Mufindi, Chamwino, Longido pamoja na Wilaya ya Maswa.

 

MWISHO.

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post