Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha (wa pili kushoto) akitoa taarifa ya Mradi wa Maji Kijiji Cha Zabazaba kwa Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo (wa kwanza kulia).
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo (mwenye shati jeupe katikati) akikagua moja ya kituo cha kuchotea Maji katika kijiji Cha Zabazaba wilayani Maswa.
Na Samwel Mwanga, Maswa.
MBUNGE wa Jimbo la Maswa Mashariki, Mkoa wa Simiyu Stanslaus Nyongo (CCM), ametembelea miradi ya maji katika Kata za Sukuma, Mbaragane na Masanwa ili kujionea utekelezaji wake.
Miradi hiyo ambayo inatekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira wa Mjini Maswa (MAUWASA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ili kuboresha hali ya maisha.
Ziara hiyo ya siku mbili katika jimbo hilo pia imewashirikisha maafisa kutoka Halmashauri ya wilaya, MAUWASA na RUWASA.
Miradi aliyotembelea ni pamoja na Ujenzi wa tenki la kuhifadhia Maji lenye ukubwa wa Lita Milioni mbili linalojengwa na MAUWASA katika Kijiji Cha Hinduki, Kata ya Sukuma kwa gharama ya shilingi Bil. 2,243,878,254.25
Miradi mingine ni mradi wa Maji wa Kijiji Cha Zabazaba wenye thamani ya shilingi mil. 323,924,717.55 ulioko katika Kata ya Sukuma, Mradi wa maji kijiji Cha Sulu, kata ya Mbaragane wenye thamani ya Sh 384,104,785,29 na Mradi wa maji kijiji Cha Masanwa wenye thamani ya Sh 409,717,169 na miradi yote hii inatekelezwa na RUWASA.
Akizungumza katika ziara hiyo Nyongo amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Wananchi wanapata huduma ya Maji safi na salama pamoja na kumtua mama ndoa kichwani na kumpunguzia umbali wa kwenda kutafuta Maji na badala yake kumuongezea muda kufanya shughuli zingine za maendeleo Ili kujiimarisha kiuchumi na kijamii.
Mbunge Nyongo ameipongeza MAUWASA na RUWASA wilayani humo kwa kusimamia vizuri miradi wa maji yote inayoletwa katika wilaya ya Maswa hususani katika jimbo la Maswa Mashariki.
Amesema kuwa ni vizuri kwa Taasisi hizo zinazoshughulikia masuala ya Maji ni vizuri kuhakikisha wanatumia vizuri fedha zilizotolewa na Serikali ya awamu ya sita kwa ajili kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi sambamba na kumtua mama ndoo kichwani.
"Nawapongeza wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya Maji iliyoko katika jimbo la Maswa Mashariki kupitia Mauwasa na Ruwasa kwa usimamizi mzuri, miradi imekuwa na matokeo mazuri kama ule Mradi wa Kijiji Cha Sulu na lengo la Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuleta fedha nyingi katika sekta ya Maji ni kutaka kuona fedha zinaleta matokeo makubwa na kuondokana na tatizo la maji,"
"Licha ya kwamba miradi hii ya maji ya Kijiji Cha Sulu na Kijiji Cha Masanwa kukamilika na kuanza kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yao umeshaanza kuwanufaisha wananchi tunachohitaji kuona sasa zile changamoto ndogondogo zilizopo kama vile kuongeza Vituo vya kuchotea maji zinamalizika katika miradi hiyo,"amesema.
Nyongo amewataka viongozi wa vijiji pamoja na wananchi kushirikiana kulinda miundombinu ya maji huku akiziagiza Jumuiya za watumiaji maji kukusanya fedha na kutumia fedha kwa ajili ya uendelevu wa mradi wa maji.
"Hongereni kwa kupata maji safi na salama Wananchi wa maeneo miradi ambayo imekamilika na Jukumu lililobaki sasa ni kutunza miundombinu ya maji hii miradi ni mali yenu wananchii na imewapunguzia adha ya kutafuta maji kwa umbali mrefu hasa wakina mama hivyo itunzeni miradi hii nami nawahaidi kuendelea kutafuta fedha serikali Ili kuhakikisha Jimbo letu tunapunguza au kumaliza tatizo la upatikaji wa Maji katika maeneo hasa ya vijijini,"amesema.
Naye Meneja wa Ruwasa wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha amesema kuwa wataendelea kusimamia kwa umakini utekelezaji wa miradi yote ya Maji na uibuaji wa vyanzo vipya vya Maji katika wilaya hiyo chini ya Ruwasa
Mhandisi Madaha ameishukuru serikali kupitia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Kwa kutoa fedha nyingi Ili kutekeleza Ilani ya CCM ya kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 85 maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2025.
Mwisho.
Post a Comment