Na
Derick Milton, Nyakabindi.
Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI)
imewasisitiza wakulima katika kipindi hiki ambacho Mamlaka ya hali ya hewa
nchini imetangaza kuwepo kwa mvua chache zitakazonyesha, kutumia mbegu zinazozalishwa
na kituo hicho ambazo zinastahimili ukame.
Aidha wakulima wametakiwa kuzitumia mvua hizo kwa
manufaa, kwa kutumia teknologia zinazoendana na hali ya hewa hiyo ambazo nyingi
zinapatika kwenye vituo vyake vya umahili vya usambazaji teknologia za kisasa.
Wito huo umetolewa na Dkt. George Sonda Mratibu wa
uhaulishaji wa teknologia kutoka TARI ukiriguru mkoani Mwanza, wakati
akizungumza na wakulima mkoani Simiyu kwenye kituo cha umahili cha usambazaji
wa teknologia za kisasa TARI Nyakabindi kwenye siku ya mkulima.
Dkt. Sonda amesema kuwa ni wakati sasa wakulima
kutumia mvua hizi chache kwa umakini, kwa kutumia teknologia za kisasa ili
waweze kuzalisha kwa tija, ikiwemo kupanda mazao kama mtama, mihogo ambayo
yanayostahimili ukame.
“ Tunawasisitiza wakulima na kuwashauri sana
katika hali hii ya mvua chache zilizotangazwa, tutumie vituo vyetu vya TARI
kupata teknologia ambazo zitatusaidia kuzalisha kwa tija,” amesema Dkt. Sonda…..
“ Vituo vyetu vyote kikiwemo hiki cha Nyakabindi,
vina teknologia za kutosha, tunawashauri wakulima watumie hivi vituo kuja
kuchukua mbegu bora ambazo zinaweza kupambana na ukame, magonjwa, lakini zenye
mavuno mengi,” aliongeza Dk. Sonda.
Mtafiti kutoka TARI tumbi Mkoani Tabora Martha
Ndelemba, amewashauri wakulima kwenye kipindi hiki kulima zao la mtama kwa
kutumia mbegu bora aina ya TARISO TWO inayastahimili ukame na mazao yake ni
mengi.
“ Kwa sasa TARI tuna mbegu bora ya zao la Mtama,
inaitwa TARISO TWO, wakulima tunawashauri kwa kipindi hiki watumie mbegu hii,
inastahimili ukame, mazao yake ni mengi lakini pia ustahimili mashambulizi ya
magonjwa” amesema Ndelemba.
Ofisa Mfawidhi wa
kituo hicho cha Nyakabindi Isabela Mrema amesema tangu kituo kianzishwe
toka mwaka 2021, jumla ya wakulima 3,121 wanawake wakiwa 750 na wanaume 2,371
wamepewa mafunzo ya teknologia za kisasa.
Isabela amesema
kuwa mwitikio wa wakulima kuja kwenye kituo hicho umekuwa mkubwa, ikiwemo
vijana kutembelea kituo hicho kwa ajili ya kujifunza teknologia za kisasa na
kuchukua mbegu bora.
MWISHO.
Post a Comment