Na
Derick Milton, Nyakabindi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahya Nawanda
amewataka wakulima mkoani humo, kuhakikisha wanatunza chakula katika kipindi
hiki kwani uzalishaji utakuwa mdogo kutokana na hali ya hewa.
Dkt. Nawanda amesema kuwa kutokana na mvua kuwa
chache na uzalishaji wa mazao kuonekana kuwa mdogo, amewataka wakulima kwa
mazao ambayo watavuna kuyatuza kwa ajili ya familia zao wakiwemo watoto.
Mkuu huyo wa mkoa amezungumza hayo jana, akiwa na
wakulima kwenye kituo cha umahili cha usambazaji teknologia za kisasa za kilimo
TARI Nyakabindi wakati wa siku ya mkulima shambani.
Amesema kuwa kutokana na hali hiyo, wakulima
hawana budi kuacha kuanza kuuza chakula, na badala yake wakitunze ili kuweza
kukitumia wao pamoja na familia zao kwani uzalishaji utakuwa kidogo.
Amewataka wakulima kutouza chakula chote
walichonacho, na badala yake wakitunze ili kije kuwasaidia mbeleni ikiwa
kutakuwepo na upungufu wa chakula nchini.
“ Niwaombe wakulima wa mkoa wa Simiyu, tutunze chakula
ambacho tumezalisha mwaka huu, hali ya hewa siyo mzuri na uzalishaji ni mdogo,
hivyo sasa tutunze hiki chakula, tusiuze, tukitunze kwa ajili ya familia zetu,”
amesema Dkt. Nawanda.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa
amewasisitiza wakulima kutumia vyema uwepo wa kituo cha TARI Nyakabindi mkoani
humo, kwani kinazalisha teknologia nyingi za kisasa za kilimo ikiwemo mbegu
bora.
Amewataka watalaamu kwenye kituo hicho,
kuhakikisha wakulima wengi zaidi mkoani humo wanafika kituoni hapo kwa ajili ya
kujifunza ikiwa pamoja na kupewa mbegu bora za kisasa ili waweze kuzalisha kwa
tija.
Nao wakulima waliohudhulia siku hiyo,
wamekipongeza kituo hicho kwani kimewabadilishia maisha kwa kuwafundisha njia
bora za kilimo cha kisasa kuliko ilivyokuwa zamani.
Wakulima hao wamesema kuwa uwepo wa kituo hicho,
wamenufaika kwa kiwango kikubwa, kwani ujifunza kila wakati namna bora ya
kuzalisha kwa tija ikiwa pamoja na kupatiwa mbegu bora zilizofanyiwa utafiti.
“ Kama wakulima tumenufaika kwa kiwango kikubwa na
kituo hiki tangu kimeanzishwa, tumepata elimu, mbegu bora, tulikuwa tunalima
kwa mazoea lakini kwa sasa tunalima kisasa, na kwa tija,” amesema Elia Elisha
Mkulima.
Hata hivyo wakulima wameiomba serikali kutatua
changamoto ambayo inakikabili kituo hicho ya upatikanaji wa maji ya uhakika,
kwa kichimba kisima kirefu ambacho kitazalisha maji muda wote.
Naye Mratibu wa uhaulishaji wa teknologia kutoka
TARI ukiriguru mkoani Mwanza Dkt. George Sonda , amewasisitiza wakulima katika
kipindi hiki ambacho Mamlaka ya hali ya hewa nchini imetangaza kuwepo kwa mvua
chache zitakazonyesha, kutumia mbegu zinazozalishwa na kituo hicho ambazo
zinastahimili ukame.
Ofisa Mfawidhi wa
kituo hicho cha Nyakabindi Isabela Mrema amesema tangu kituo kianzishwe
toka mwaka 2021, jumla ya wakulima 3,121 wanawake wakiwa 750 na wanaume 2,371
wamepewa mafunzo ya teknologia za kisasa.
MWISHO.
Post a Comment