Dc aridhishwa na Utekelezaji Miradi ya Maji MAUWASA.

MKUU wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Aswege Kaminyoge akitoa maelekezo wakati akikagua ujenzi wa Tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita milioni mbili linalojengwa katika kijiji cha Hinduki wilayani humo.

 
Mkuu wa wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge (mwenye shati jeupe) pamoja na kamati ya Ulinzi na Usalama wakipokea taarifa ya ujenzi wa tenki la Kuhifadhia maji lita mil. 2 linalojengwa kijiji cha Hinduki, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (MAUWASA).

 

 
Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.

MKUU wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama wamesema wameridhishwa na Ujenzi wa miradi ya Maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MAUWASA) kwamba inaendana na thamani ya fedha.

 

Aidha Kaminyoge amesema ameridhika na matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali katika miradi ya maji na kwamba fedha za kutekeleza miradi hiyo zimekuwa hazikai kwenye akaunti kwa muda mrefu pindi zinapotolewa na serikali.

 

Ameyasema hayo juzi wakati akikagua ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita milioni mbili lilioko kijiji cha Hinduki na ulazaji wa bomba katika tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja lililoko mjini Maswa.

 

Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia imetoa zaidi ya Bil. 2 kwa ajili ya ujenzi wa tenki la maji kwa ajili ya kutoa huduma ya maji kwa wananchi katika mji wa Maswa.

 

‘’Mradi huu ukikamilika, wananchi wa Mji wa Maswa watapata maji kwa masaa 24 tofauti na ilivyo sasa wanapata maji kwa masaa 8…ninamwaomba Rais Samia na Waziri wa Maji (Jumaa Aweso) waendelee kutoa fedha ili kukamilisha miradi ya maji’’ alisema Kaminyoge.

 

Alifafanua kuwa mradi huo ukikamilika, wananchi watapa maji kwa uhakika na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira itapunguza nusu ya gharama za umeme za usambazaji wa maji kutoka milioni 25 kwa mwezi hadi kufikia milioni 10 au 12.

 

Aliwaonya wananchi kutohujumu miradi ya maji kwa kukata mabomba na endapo watabainika kufanya uhalifu, viongozi wa eneo hilo watachukuliwa hatua za kisheria kwani wanatakiwa kuwa walinzi wa miradi ya maji sababu inawanufaisha wananchi moja kwa moja.

 

Awali  Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) Mhandisi Nandi Mathias alisema wameanza kutekeleza ahadi ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ya Ujenzi wa tenki la kuhifadhi Maji lita Milioni mbili na ulazaji wa bomba katika tenki la Maji lenye ujazo wa lita Milioni moja.

 

Mhandisi Nandi Mathias alisema kuwa tayari wameshapokea kiasi cha fedha zaidi ya shilingi Mil. 350 Kwa ajili ya Ujenzi wa tenki hilo ambalo limeshaanza kujengwa katika Kijiji Cha Hinduki.

 

Mhandisi Nandi alisema pia tayari wameshanunua bomba zenye gharama ya shilingi mil. 250 na kazi ya ulazaji wa bomba katika tenki jipya lililoko kwenye kilima cha Nyalikungu mjini Maswa umeshaanza ambalo Lina uwezo wa kuhifadhi Maji lita Milioni moja.


 
"Mtakumbuka kuwa Waziri Aweso alifanya ziara katika Mamlaka yetu ya Mauwasa aliweza kuzindua ule mtambo wa kutibu na kuchuja Maji ambao ni mkubwa sana uliko katika Kijiji Cha Zanzui" alisema Mhandisi Nandi.

 
Alisema kuwa pindi miradi yote hiyo itakapokamilika itawasaidia wakazi wa mji wa Maswa na vijiji 11 wanaotumia maji kupitia chanzo Cha maji Cha bwawa la New Sola watapata maji ya uhakika kwa muda wa masaa 24 sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji kwa mamlaka hiyo.

 
"Kwa Sasa Wananchi tunaowahudumia wanapata Maji kwa masaa 12 lakini baada ya Ujenzi wa tenki lile tunalojenga huko Hinduki ukikamilika na hili tenki lililojengwa kwenye kilima cha Nyalikungu likaanza kazi hivyo Wananchi watapata maji Kwa masaa 24,"amesema.

 
Mhandisi Nandi alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru  Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuruhusu kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo inayosimamiwa na Mamlaka hiyo kupitia Wizara ya Maji.

MWISHO.

 

  Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (MAUWASA) Mhandisi Nandi Mathias kipanda ngazi kwa ajili ya kukagua ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita mil. 2 linalojengwa kijiji cha Hinduki wilayani Maswa.


Ulazaji wa Mabomba katika tenki jipya lililoko kilima cha Nyalikungu mjini Maswa unaendelea katika tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita milioni moja.


Ujenzi wa Tenki la Kuhifadhia Maji lenye ujazo wa lita milioni mbili ukiendelea katika kijiji cha Hinduki wilaya Maswa mkoani Simiyu.



 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم