Dk. Nawanda amewataka watumishi wa Umma kuacha tabia ya kukopa ovyoovyo na badala yake watumie mabenki kuomba Mikopo ambayo Haina masharti magumu.
Mkuu huyo wa Mkoa ameyasema hayo leo kwenye maadhimisho ya sikukuu ya Wafanyakazi yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya mpira wa miguu Lamadi wilayani Busega.
Aliwataka Maafisa Utumishi na Wakurugenzi kudhibiti kampuni za Mikopo zinazoumiza watumishi wa Umma na kuongeza kuwa hakuna mtumishi anayetatua Maisha yake Kwa kukopa.
"Twendeni tukakope kwenye mabenki yanayotambulika na wale wanaopitisha Mikopo umiza tutaanza kuwashughulikia....Nawaomba tukope kulingana na sheria za Utumishi wa Umma zinavyotaka, kopeni kwenye mifumo yenye staha na stara" Alisema Dk. Nawanda.
Amemwagiza Katibu Tawala pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu kukaa chini na Wakuu wa mashirika ili kuangalia kwenye kanzi data ya watumishi waliokopa kupitiliza ili waweze kujua aliyepitiliza mkopo nani alihusika kuupitisha.
Katika hatua nyingine Dk. Nawanda amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia itaendelea kusimamia na kuboresha maslahi ya watumishi wa Umma kadri ya bajeti itakavyoruhusu.
Amesema serikali itaendelea kumlinda mtumishi wa Umma mahali pa kazi huku akiwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanatatua kero za watumishi wa Umma zilizondani ya uwezo wao ikiwemo malipo ya fedha za likizo.
"Wanaostahili kwenda Likizo waende, anayedai fedha za likizo apewe...Katibu Tawala hakikisha hili linafanyika mara moja na Wakuu wa idara tendeni Haki Kwa Watumishi wa Umma" amesema.
Awali akiwasilisha risala, Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoa wa Simiyu (TUCTA) Valerian Vedasto amesema wanaipongeza serikali ya awamu ya sita Kwa kutoa ajira, kupandisha madaraja watumishi na kutoa vitendea kazi Kwa Watumishi ikiwemo pikipiki na vishikwambi Kwa walimu.
Amesema ujenzi wa miundombinu ya elimu (madarasa, vyoo na nyumba za walimu), zahanati na vituo vya Afya utaongeza ufanisi Kwa Watumishi wa Umma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Simiyu Kulwa Dwese amesema tangu 2016 wafanyakazi walikuwa wamesimama kupandishwa madaraja, lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani wameanza kupandishwa madaraja.
Ameiomba serikali kurekebisha kanuni mpya za kikokotoo ambazo zinaumiza watumishi wa Umma huku akisema kanuni za zamani za kikokotoo zilikuwa na unafuu Kwa Watumishi wa Umma.
MWISHO.
Wafanyakazi kutoka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Mkoa wa Simiyu wakipita mbele ya mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi yaliyofanyika Lamadi-Busega, mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda.
إرسال تعليق