Madiwani Bariadi Mji waipongeza TASAF kuboresha miundombinu.

 

Mwenyekiti wa Halmashauri wa Mji wa Bariadi David Masanja (katikati) akiongoza kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika ukumbi wa Bariadi Mji, kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Kija Bulenya, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Adrian Jungu.


 Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu limeupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya Elimu, Afya na Barabara.

 

Aidha, wamesema licha ya mfuko huo kushirikisha wananchi moja kwa moja, umesaidia kuimarisha utoaji wa huduma kwa kujenga zahanati, mabweni, vyumba vya madarasa, maktaba, na barabara.

 

Hayo yamebainishwa leo na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo David Masanja kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya mji ulioko Nyaumata.

 

Masanja amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia miradi ya OPEC imekuwa mkombozi kwenye maeneo yao ambapo wananchi wananufaika moja kwa moja kupitia ajira za muda wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

 

Mwenyekiti huyo amewataka Madiwani kuhakikisha wanasimamia miradi ya TASAF na pia kuwahimiza wananchi kuchangia asilimia 10 ya miradi hiyo kwa kutoa nguvu kazi ikiwemo kusomba mawe na mchanga, kuwagilia maji, kusafisha maeneo, na kuchimba msingi.

 

‘’TASAF amekuwa mkombozi sana kwenye maeneo yetu, naomba tuhimize wananchi wetu wajitoe kuchangia asilimia 10 ili tuweze kufikia vigezo vya kupata miradi…kwenye kata yangu ya Nyakabindi wanejenga zahanati mbili na kufungua barabara’’ alisema Masanja.

 

Awali akitoa elimu na miongozi juu ya utekelezaji wa miradi ya TASAF kupitia OPEC, mbele ya Madiwani, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Idara na wadau wengine, Mshauri wa TASAF wilaya ya Bariadi Lucas Mkwizu amesema miradi hiyo imelenga kuwanufanisha wananchi moja kwa moja.

 

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unawahitaji wananchi wa eneo husika kwa kuchangia asilimia 10 ya ujenzi kupitia kujitolea nguvu kazi ili kuleta umiliki wa miradi hiyo moja kwa moja.

’Miradi ya TASAF inayofadhiliwa na OPEC, inahitaji wanachi wachangie asilimia 10 ya nguvu kazi na siyo fedha…miradi hii hainafanani na miradi mingine inayoletwa na serikali kama ya Boost ambapo mradi unafadhiliwa hadi kukamilika’’ alisema Mkwizu.

 

Amewataka Madiwani kutumia nafasi zao kuwahamasisha wananchi kushiriki ipasavyo kuchangia miradi hiyo ili iweze kuwanufaisha na kuwapunguza adha ya ukosefu wa miundombinu.

 

Amesema kupitia ufadhili wa OPEC, TASAF wanajenga madaraja, mabweni, majengo ya utawala kwenye shule za sekondari, maktaba, barabara, zahanati na kutoa ajira za muda kwa walengwa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

 

MWISHO.

 

Mshauri wa TASAF wilaya ya Bariadi Lucas Mkwizu akitoa elimu kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi juu ya utekelezaji wa miradi ya TASAF chini ya ufadhili wa OPEC.


Madiwani wa Halmashauri wa Mji wa Bariadi wakiwa kwenye kikao.


Madiwani wakiendelea na kikao.
 
 
Mshauri wa TASAF wilaya ya Bariadi, Lucas Mkwizu akitoa elimu kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi David Masanja (wa pili kushoto) akiongoza kikao cha Baraza la Madiwani, kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Adrian Jungu, kulia ni Kaimu Katibu wa CCM wilaya ya Bariadi Haji Kianga na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Kija Bulenya.
 
 
Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wakifuatilia kikao cha Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
 
 
 
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post