![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhn7XHPNTZBPJFQJFUUb4LRtPROoVgsJVLd8Wa1J191ui5KUhpUcTsDVYJa38ysZFmHxtrxORGv8-9gObCb4ri0mF5pOxvOCq52xce3u94NJXKOOVwih-PtKeEDtitDYU50rZSCgNW9sQ38TDc-J3TR90E8tVRMIppwvpu6cCvrlV-rkUKrOL7musmN7ACw/w640-h426/diwani.jpg)
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wameionya na kuitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bariadi (BARUWASA) kujitathimini juu ya utoaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa mji wa Bariadi.
Aidha, Madiwani hao wameiomba serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuhakikisha wanadhibiti bei za maji zinazotolewa kwa watumiaji licha ya kutopata huduma hiyo kwa uhakika.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kujadili taarifa za maendeleo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo David Masanja ameiomba BARUWASA kujitathimini juu ya utendaji kazi vinginevyo watafikisha malalamiko hayo Wizara ya Maji.
Anasema huduma ya maji kwa wananchi wa Mji wa Bariadi hairidhishi, lakini pia upatikanaji wa maji ni wa mgao na pia bili za maji zinazotolewa ni kubwa ambazo hazilingani na huduma wanayopata.
‘’Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Mjini na Vijijini (RUWASA) wamewakabidhi BARUWASA visima na manteki ya maji kwa ajili ya kuongeza utoaji wa huduma ya maji…lakini bado wanasuasua, tunawaomba sana wajitathimini vinginevyo tutaiomba Wizara ya Maji kuwaondoa watumishi ili ilete wengine’’ anasema Masanja.
Diwani wa Kata ya Bunamhala Nkamba Zabron anasema Mamlaka hiyo ilikuwa unahudumia kata nne za mji wa Bariadi ambazo ni Malambo, Sima, Bariadi na Somanda lakini wameshindwa kuzihudumia ipasavyo.
‘’tumewaambia wajithamini kwa sababu wanakwenda kuongezewa nguvu nyingine, tunaona wanapwaya kuhudumia wananchi…hivyo wajitathimini kwa sababu wananchi wanapata changamoto ya kutopata maji mara kwa mara na pia maji kutoka saa saba usiku na bili ni kubwa tofauti na matumizi’’ anasema Nkamba.
Diwani wa Viti Maalumu, Juliana Lucas anaitaka BARUWASA kujitathimini ili wasiiangushe serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imejikita kuimarisha huduma za maji mjini va vijiji ili kumtua mama ndoo kichwani.
Akitolea ufafanuzi malalamiko hayo, Meneja Ufundi kutoka BARUWASA, Chadwick Mbunde anasema taasisi hiyo ina leseni ya kutoa huduma ya maji katika eneo lote la mji wa Bariadi yenye kata 10.
‘’tuko kwenye mchakato wa kukabidhiwa miradi hiyo kwenye kata sita ili tuweze kuendesha miradi yote katika kata zote 10, changamoto kubwa katika mji wa Bariadi ni uhaba wa vyanzo vya maji, huu mji unakuwa kwa kasi sana’’ anasema.
Anafafanua kuwa vyanzo vya maji vilivyopo havijitoshelezi sababu vina uwezo mdogo wa uzalishaji wa maji ikilinganishwa na mahitaji ya maji kwa siku ambapo kwa wastani visima hivyo vina uwezo wa kuzalisha lita milioni 4 kwa siku lakini mahitaji ya watu ni lita milioni 9 kwa siku.
Anasema Mamlaka hiyo inazitambua changamoto zinazowakabili wananchi na wanazo njia za muda mfupi na mrefu kwa ajili ya kutatua changamoto ikiwemo kuendelea kuongeza visima na kwa sasa wana visima 27.
‘’tunaendelea kuongeza visima vingine zaidi ili kuongeza uzalishaji wa maji, tuna mipango ya kutanua mtandao wa amji ili kuyafikia maeneo ambao hayajafikiwa na huduma ya maji’’ anasema.
Anaongeza kuwa wanaongeza kilometa 42 za mtandao wa maji na wamechimba visima virefu vitatu ambavyo vitaongeza wingi wa maji na katika mpango wa 2023/24 wamepanga kuongeza kuchimba visima vitano ili kuongeza upatikani wa maji.
MWISHO.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiOEsO3U93yY8-FDDsTl7iA1j-jPrrtYEp9N5ddmC3m8OwYJSBkYS66RRr9dB4snu1VDSbTpL92qDV_K6vU6T87VAeSj57DidlLfc9f_en2Ud2JrKTZ-xLQewlO0rvLqawbit8yX_S52WoSljqY7GYVCoROVZalFoDiZ6jsqKOQ_Og5hD4ksWYlj4H4q0kD/w640-h426/baruwasa%202.jpg)
إرسال تعليق